Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Mikopo ya kausha damu ama mikopo umiza siku za hivi karibuni zimeshika kasi katika maeneo mengi nchini kutokana na urahisi wa upatikanaji wake.Wateje wakubwa wa mikopo hii ni wafanyabiashara ndogo ndogo na baadhi ya wafanyakazi ambao wamegeuza fadha hizi kama njia ya kujiatulia matatizo yao ya kifedha kwa uharaka zaidi bila kufuata mlolongo wa masharti ya kukopeshwa.
Pamoja na umuhimu wake kwa baadhi ya watu bado ni mwiba ambao kwa Yule mkopeshwaji ambaye amechelewa kulipa humchoma kwa kumdhalilisha kwa namna ambayo hakutarajia kama vile kuuziwa mali zake,kufuatwa sehemu ya kazi,na hata vitisho hali ambayo inashusha utu wa mtu.
Licha ya watu kuzifahamu changamoto hizo bado makampuni ya ukopeshaji yanaongezeka na wateja wanakimbilia moja kati ya sababu za ongezeko hilo ni kile kinachotajwa kuwa ni kupanda thamani ya maisha na kufanya maisha kuwa magumu.

Hivi karibuni katika kijiji cha Mwandobana wilayani Bariadi mkoani Simiyu Kija Masanja alikutwa katika hali ngumu baada ya kukopa fedha kiasi cha shilingi milioni moja kwa Kuhi Nduhye ambaye makubaliano yalikuwa kulipa milioni mbili kwa dhamana ya shamba la ekari nne, shamba ambalo Nduhi aliliuza kwa milioni 5 na kuondoka na pesa zote baada ya Kija kushindwa kumlipa milioni moja hali ambayo serikali ikaingilia kati, ili kurudisha mali hiyo.
Kufuatia tukio hilo na yale yanayoendana na hilo, Jambo Fm imezungumza na wakazi wa Bariadi ambao wamesema wanatamani kuona kila mtu akijishughulisha na kazi kwa bidii na kuachana na mikopo hiyo iliyo na riba kubwa na inayowarudisha katika umasikini.
“Unaweza ukakopa shilingi laki 5 lakini ndani mwako hauna vitu vya kukufanya ulipe hiyo pesa ikafika kipindi ambacho biashara imekuwa ngumu marejesho umekosa wale watu huwa hawaangalii wakija kwako watachukua kila kitu haijalishi una watoto ama vipi, majirani wanaona sasa ukifikiria hilo ni bora hata ufanye kilimo upate kidogo kuliko kausha damu,” amesema Macklina Julius mkazi wa Bariadi.
Husna Mashurubu ni mnufaika wa mikopo ya halmsahauri ambaye alipita katika mikopo ya kausha damu anasema kuwa haikuwa rahisi kuimaliza kwani walilazimika kulipa riba kubwa isiyoendna na pesa waliyoichukua.
“Nilipoanza kazi ya mama lishe sikuwa na vyombo na mtaji wa kununua vyakula hivyo nikaingia kausha damu,kila jioni nawaza natoa wapi rejesho nilichukua laki nane marejesho ukihesabu unakaribia kulipa mara mbili ya pesa uliyoichukua ,ambacho kinafanya watu waone wepesi ni pesa ndogo ya kila siku lakini ukipiga hesabu unagundua umewanufaisha wao, walikula sana faida ya kazi yangu,” amesema Husna mama lishe Nyamimbi.
“Mimi naona mabadiliko yaanzie kwetu tuhame katika mikopo ya namna hii hawa wakopeshaji wakikosa wateja ambao ni sisi makampuni yatapungua, tuanze kuangalia taasisi za kifedha ambazo zinakuhitaji uwe na mali za kukopesheka na ambazo hazitoathiriwa na kile utakachokopa au twende kwenye pesa za serikali huo ndio ushauri wangu kwa wana Bariadi,” alisema.
Discussion
Reader comments
0 contributions