Skip to main content

MIGONGANO SEKTA YA MADINI: WATAALAMU, WADAU WAIOMBA NEMC KUWA NA KITUO JUMUISHI

Na Ibrahim Rojala - Geita.

MIGONGANO SEKTA YA MADINI: WATAALAMU, WADAU WAIOMBA NEMC KUWA NA KITUO JUMUISHI

Na Ibrahim Rojala - Geita.

Watalamu na wadau wa mazingira nchini, wameiomba Serikali kupitia baraza la uhifadhi na usimamizi wa Mazingira NEMC, kuwa na kituo jumuishi kitakachowaleta pamoja wadau wa mazingira na taasisi, ili kuondoa migongano iliyopo ambayo imekuwa ikiathiri uwekezaji katika Sekta ya madini.

Ombi hilo, limetolewa  Aprili 17, 2026 katika kikao kilichoandaliwa na NEMC kanda ya ziwa Viktoria Magharibi inayoungwa na mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera pamoja na wadau na watalamu wa mazingira, kilichokuwa na lengo la kujadili kero zinazowakabili wadau hao.

Kwa mujibu wa wadau hao, wameeleza kuwa kutokana na kuwepo kwa mwingiliano wa kisheria baina ya NEMC na tume ya madini katika usimamizi wa Sheria  za mazingira nchini,imekuwa ikichelewesha miradi na kuongeza gharama katika uwekezaji kupitia mchakato mrefu uliopo wakati wa kupata vibali vya mazingira.

Mwanasheria kutoka mgodi wa Almasi Mwadui(Wiliamson Diamonds limited), Sylivia Leonidas amesema kukosekana kwa kituo jumuishi kinachotoa huduma za kimazingira, imekuwa ikiwaathiri wawekezaji mathalani katika sekta ya madini ambao hutakiwa kutekeleza kanuni za kimazingira.

Sylivia amesema wawekezaji hasa katika Sekta ya madini pindi wanapokuwa katika harakati za kianzishwa na uendeshaji, inaongeza gharama kutokana na kuwa na michakato inayowataka kupita taasisi mbalimbali za kiserikali kama NEMC, Tume ya madini, TMDA, GCLA hali inayoongeza mlolongo wa kiuwekezaji,hivyo kushauri kuwa na kituo jumuishi kitakachokuwa na jukumu la pamoja katika kutoa huduma.

Naye Mtalamu na mshauri wa Mazingira, Frank James ameishukuru NEMC kuandaa kongamano hilo jumuishi la wadau na kushauri mamlaka hiyo kufanya mwendelezo wa vikao na wadau itakayowawezesha wadau wa mazingira na watalamu katika kusimamia na kutekeleza sheria za kimazingira katika maeneo yao ya uwekezaji kupitia kituo jumuishi.

Aidha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Geita, Leonard Bugomola,amesema licha ya kuwepo kwa mchakato mrefu kwenye upatikanaji wa vibali vya mazingira,ameishukuru Serikali kupitia NEMC kutokana na kuanzishwa kwa utaratibu wa utoaji elimu kwa wawekezaji badala ya kuwafungia ambapo kwasasa kero ya kufungiwa imepungua tofauti na zamani.

Kufuatia mapendekezo ya wadau,Meneja wa Baraza la uhifadhi wa Mazingira (NEMC),kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Boniphace Guni ameahidi kulifikisha suala hilo katika ngazi za juu kwaajili ya mapitio ya Sheria hiyo ili kuendelea kuvutia uwekezaji huku akiahidi mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi.

“Kumekuwa na changamoto ya upataji vibali kutoka katika mamlaka ambazo wakati mwingine hazina dhamana hiyo,hii yote inaleta mkanganyiko hasa kwa wananchi wetu pale wanapohtaji kutupa taka hatarishi ambazo zina madhara kwa jamii na mazingira”amesema

Pia NEMC limeahidi kuendelea kutoa elimu kwa watalamu elekezi wa mazingira nchini,ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao ili kuongeza uelewa kwa wadau na wawekezaji,katika kukabiliana na changamoto za kimazingira kabla na baada ya kuanza uwekezaji.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.