Na Saulo Stephen - Singida.
Katika kuharakisha safari ya Mkoa wa Singida kufikia hadhi ya Jiji na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amesema migogoro ya ardhi ni miongoni mwa vikwazo vinavyorudisha nyuma maendeleo, akitaka ikomeshwe sambamba na kuimarishwa kwa usimamizi wa taka, ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na nidhamu ya utendaji ili kufikia malengo ya kitaifa.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Dendego alisema mafanikio ya manispaa kufikia hoja za tarakimu moja yanaonesha kuwa safari ya kuelekea Jiji la Singida imeanza.

Dendego amesisitiza kuwa ufundi si kujibu hoja bali kuzizuia, huku akitaka watumishi wanaozalisha hoja kuwajibishwa kisheria.
Amesema, "tusikubali migogoro ya ardhi iturudishe nyuma. Tumeanza safari ya Jiji la Singida, sasa tuongeze kasi, tuwe wabunifu kwenye mapato, tuweke mazingira safi na tufikie Dira ya 2050."

Aidha, ameagiza migogoro ya ardhi iliyopo itatuliwe haraka bila kuzalisha mingine, taka zichakatwe kuwa fursa za kiuchumi, na viongozi waendelee kusimamia ustaarabu, uwajibikaji na huduma kwa wananchi.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Mhe. Geofrey Shaban Mdama, amesema madiwani wamejipanga kuongeza ukusanyaji wa mapato na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa karibu ili kufanikisha ndoto ya Jiji la Singida. Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, amesema wilaya itaendelea kushirikiana na manispaa kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Bi. Joanfaith Kataraia, amesema manispaa imeendelea kutekeleza mapendekezo ya CAG na maagizo ya Kamati za Fedha, huku ikisimamia miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Kikao hicho kilibaini kuwa mafanikio ya kufikia Single Digits ni msingi muhimu wa kujenga Manispaa yenye ushindani, kuongeza mapato na kuifanya Singida kuwa miongoni mwa maeneo yenye maendeleo ya mfano kitaifa.
Discussion
Reader comments
0 contributions