Na Daniel Gahu – Katavi.
Hatimaye, mwanamke mwenye umri wa miaka 80 anayejulikana kwa jina la Hamisa Salum amepata matibabu ya kibingwa ya ugonjwa wa fistula katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, baada ya kuishi na tatizo hilo kwa takribani miaka 60.
Mwanamke huyo alipata fistula akiwa na umri wa miaka 20, lakini kwa muda wote huo hakuweza kupata matibabu ya kibingwa hadi ujio wa madaktari bingwa walioweka kambi maalumu ya matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda, Dkt. Paul Swakala, amesema ujio wa madaktari hao umetoa fursa muhimu kwa wananchi wenye changamoto ya fistula, akieleza kuwa tukio hilo limewezesha pia mzee huyo kupata matibabu ambayo ameyasubiri kwa miongo kadhaa.
“Ujio wa madaktari hawa ni fursa kubwa kwa wananchi wetu. Tumepata nafasi ya kumtibu Bibi huyu mwenye miaka 80 ambaye amekuwa akiishi na fistula tangu akiwa na miaka 20,” amesema Dkt. Swakala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph, amewataka wananchi wenye changamoto ya fistula kujitokeza kupata huduma katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, akisisitiza kuwa matibabu hayo yanatolewa bure bila gharama yoyote.
Amesema wanawake wanaopata fistula wakati wa kujifungua wanapaswa kutafuta matibabu mapema ili kurejesha afya zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

“Huduma hizi ni bure. Wananchi wenye changamoto ya fistula wajitokeze kwa wingi kupata matibabu na kutumia fursa hii muhimu ya kuwepo kwa madaktari bingwa hapa Mpanda,” amesema Mhe. Jamila.
Ameongeza kuwa, uwepo wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata matibabu.

Naye Dkt. Haule, Daktari Bingwa aliyebobea katika matibabu ya fistula nchini, amesema wagonjwa wanaopatiwa huduma katika kambi hiyo hawatozwi gharama yoyote.
Ametoa wito kwa wagonjwa kufuata kikamilifu ushauri na maelekezo ya wataalamu wa afya kabla na baada ya matibabu ili kuongeza uwezekano wa kupona vizuri.

Kwa miaka 60, fistula ilikuwa sehemu ya maisha ya mwanamke huyo, tangu akiwa kijana wa miaka 20 hadi kufikia umri wa miaka 80.
Matibabu aliyoyapata sasa yanafungua ukurasa mpya wa maisha yake, huku tukio hilo likitoa ujumbe muhimu kwa wananchi wengine wenye changamoto kama hiyo kwamba fistula inaweza kutibiwa na si lazima mtu aishi nayo maisha yote.

Wananchi wenye changamoto ya fistula katika Wilaya ya Mpanda wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa madaktari bingwa na kufika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Discussion
Reader comments
0 contributions