Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mutasingwa, amesema ataendelea kutekeleza ahadi yake ya kuendeleza sekta ya michezo kwa kugawa vifaa vya michezo katika kata zote za jimbo hilo , li kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii.
Mutasingwa aliyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu saba za mpira wa miguu katika Kata ya Kashai, ambapo aliwataka vijana waliopokea vifaa hivyo kuvitumia kwa nidhamu, kujituma katika mazoezi na kutumia michezo kama daraja la kufikia ndoto zao za kucheza katika viwango vya juu.

Alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila ushirikiano, umoja na mshikamano kati ya viongozi na wananchi, huku akiwashukuru viongozi wa Serikali, viongozi wa chama na wananchi kwa kuendelea kumuunga mkono katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, alisema Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na viongozi na wadau wote wanaotekeleza shughuli za maendeleo zinazowanufaisha wananchi, hususan vijana.

DC Sima alieleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kukuza vipaji, kuimarisha mshikamano wa jamii, kuibua fursa za ajira na kuongeza kipato kwa vijana, hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuendeleza sekta hiyo.
Ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za maendeleo ambazo Mbunge Mutasingwa alizitoa kwa wananchi wakati wa kampeni, ukilenga kuimarisha michezo ya vijana na kuongeza fursa za maendeleo katika Jimbo la Bukoba Mjini.

Discussion
Reader comments
0 contributions