Wananchi wa Kijiji cha Makuyuni, Kitongoji cha Saburi kilichopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, wametoa taarifa ya dharura na kuomba ulinzi na uingiliaji kati wa haraka kutoka kwa viongozi wa Serikali dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na mwekezaji anayeitwa Akram Aziz.
Kwa mujibu wa Wananchi wamesema mnamo Oktoba 3, 2026 mwekezaji huyo alifika kwenye kitongoji chao akiwa na tingatinga (bulldozer) kwa lengo la kubomoa nyumba zaidi ya 600, pamoja na kuharibu Misikiti, Kanisa, Shule na Zahanati.
Wamesema, kitendo hicho kilisababisha taharuki na kuzuka kwa vurugu kati yao na vibaraka wa mwekezaji huyo, wakati wakitetea haki na mali zao, jambo lililomlazimu mwekezaji kukimbia, ili kunusuru maisha yake.
Wameeleza kuwa, wamekuwa wakiishi katika Kitongoji cha Saburi kwa zaidi ya miaka 30, ambapo eneo hilo walipewa kihalali na mwekezaji aliyetangulia, na baadaye Halmashauri ilipima na kuweka alama (beacons), kutenga eneo hilo kutoka katika shamba la mwekezaji.
Wanadai eneo hilo kwasasa limetambuliwa na kusajiliwa rasmi na TAMISEMI kama Kitongoji kinachojitegemea, chenye miundombinu kamili ikiwemo shule, zahanati, misikiti na kanisa, pamoja na miundombinu ya umeme wa REA na visima vya maji.
Aidha, wananchi hao wamesema mwaka 2025 Halmashauri ilimuandikia barua rasmi mwekezaji huyo ikimtaka aachie ekari 400 ili kupisha makazi ya wananchi hao, hata hivyo mwekezaji huyo amegoma kutii agizo hilo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameiomba Serikali kupitia Ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za dharura ikiwemo kumzuia mwekezaji huyo kufanya jaribio lolote la kubomoa makazi na taasisi za kijamii katika Kitongoji cha Saburi.
Aidha, wametakakufanyika uchunguzi wa dharura kuhusu hati anazozitumia kujitwalia ardhi ya wananchi, pamoja na kulinda usalama wa maisha na mali zao kwa kupeleka vyombo vya ulinzi.
"Haiwezekani wananchi wa Kitongoji cha Saburi tuwe wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka 30. Tunaomba msaada wa haraka," wamesema wananchi hao.
Discussion
Reader comments
0 contributions