Na Saulo Stephen – Singida.
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu jijini Singida wamekabidhiwa vifaa mbalimbali vya shule vinavyolenga kuwawezesha kuendelea na masomo katika mazingira bora na kupunguza changamoto zinazowakabili kutokana na ukosefu wa mahitaji muhimu ya kujifunzia.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Godfery Madama katika hafla iliyofanyika Kanisa la God of Covenants Church, ambapo aliwataka wanafunzi hao kutumia fursa hiyo kuongeza bidii katika masomo ili kutimiza ndoto zao.

Madama alisema elimu ni msingi wa maendeleo ya mtoto na jamii kwa ujumla, hivyo kuna umuhimu wa wadau kuendelea kushirikiana kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu ili wasikose haki yao ya kupata elimu bora.
Aidha, aliwashukuru waandaaji na wadau waliofanikisha utoaji wa msaada huo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na jamii una mchango mkubwa katika kuwajengea watoto mazingira salama ya kujifunza na kufikia malengo yao ya maisha.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walionufaika pamoja na walezi wao walieleza shukrani kwa msaada huo, wakisema utawasaidia kuendelea na masomo kwa kujiamini zaidi na kuongeza ari ya kujifunza.
Discussion
Reader comments
0 contributions