Skip to main content

MAZINGIRA BORA YA ELIMU YAONGEZA MATUMAINI YA UFAULU SEKONDARI YA KAKOSO TANGANYIKA

Na Daniel Gahu - Katavi.

MAZINGIRA BORA YA ELIMU YAONGEZA MATUMAINI YA UFAULU  SEKONDARI YA KAKOSO TANGANYIKA

Na Daniel Gahu - Katavi.

Katika kuhakikisha ufaulu unaongezeka katika shule zote zilizopo katika wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amefanya ziara ya ukaguzi katika Shule ya Sekondari Kakoso kwa lengo la kujionea hali halisi ya utoaji wa elimu, maendeleo ya miundombinu pamoja na mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa wanafunzi.

Katika ziara hiyo, DC Buswelu ametembelea maeneo mbalimbali ya shule ikiwemo madarasa, mabweni na miundombinu mingine muhimu, ambapo amepata fursa ya kuzungumza na uongozi wa shule, walimu pamoja na wanafunzi kuhusu mafanikio na changamoto zinazowakabili katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Baada ya ukaguzi huo, Mkuu wa Wilaya alieleza kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa shule pamoja na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na mazingira yanayowezesha kufikia malengo yao ya kitaaluma.

Pamoja na pongezi hizo, amesisitiza umuhimu wa kuboresha lishe kwa wanafunzi akieleza kuwa chakula chenye virutubisho ni msingi muhimu wa kuongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza, kuzingatia masomo na kufanya vizuri katika mitihani. Kutokana na hilo, alielekeza shule kuanzisha bustani ya mbogamboga ili kuongeza upatikanaji wa mboga za majani na vyakula vyenye virutubisho vinavyohitajika kwa afya na maendeleo ya wanafunzi.

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya alikagua bweni la wavulana na kubaini umuhimu wa kuboresha baadhi ya maeneo ya huduma za msingi. Akiwa katika eneo la maliwato, alielekeza kufanyika kwa maboresho ya mabafu ya kuogea ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma hiyo katika mazingira salama, safi na yanayozingatia viwango vya afya na usafi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, amesema uwekezaji katika miundombinu ya shule unapaswa kwenda sambamba na kuboresha ustawi wa wanafunzi, kwani mazingira bora ya kujifunzia na kuishi yanachangia kuongeza ari ya kusoma, nidhamu pamoja na kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kakoso wameeleza kufurahishwa na hali ya upatikanaji wa chakula shuleni, wakisema lishe bora wanayoipata imekuwa kichocheo cha kuwapa nguvu za kujifunza, kuimarisha afya zao na kuongeza ari ya kufanya vizuri darasani.

Wamesema kuwa mazingira mazuri ya shule pamoja na chakula bora vinawajengea kujiamini na kuwafanya wajikite zaidi katika masomo yao, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa ufaulu wa kitaaluma.

Ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika katika Shule ya Sekondari Kakoso inaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kufuatilia na kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha shule zinakuwa na miundombinu bora, mazingira salama na huduma muhimu zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa ufanisi na kufikia ndoto zao za kitaaluma.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.