Na Ibrahim Rojala, Chato - Geita.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amemtaka Mkandarasi anaetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi 180,000 Wilayani Chato mkoani Geita kuhakikisha anakamilisha mradi huo ifikapo Septemba 30 mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, ili kuwaondolea changamoto wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Ametoa agizo hilo Julai 20,2026 akiwa katika ziara rasmi ya kikazi ya siku tano mkoani Geita yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhamasisha shughuli za kiuchumi na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Mavunde, ambaye pia ni Mlezi wa shughuli za maendeleo mkoani humo, katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Mavunde amekagua mradi huo wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 40 unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 185,000 kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama.

Baada ya ukaguzi wa mradi huo,amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya maji ili kuboresha afya za wananchi, ustawi wa jamii na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na kumtaka mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi thamani ya fedha za umma. Amesisitiza kuwa upatikanaji wa maji ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi Mjini Chato Mhandisi Isaack Mgeni amesema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 85 na kubainisha kwamba pindi utakapokamilika utakuwa na faida mbalimbali kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya maji kwa asilimia 100, kuwezesha shughuli mbalimbali za viwanda vidogo kutokana na uwepo wa maji ya uhakika na hadi sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha bilioni 23.2.
Katika kuendeleza sekta ya madini, Mavunde pia ametembelea mradi wa vijana wa ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua madini kinachomilikiwa na Kampuni ya Tampmed Limited na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchimbaji na uongezaji thamani wa madini.
Aidha, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Rwamtaba wilayanai Chato ambalo pindi ujenzi wake utakapokamilika litakarahisisha usafiri, biashara na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaendelea kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo, huku akisisitiza kuwa serikali ya mkoa imejipanga kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati ili kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza uchumi wa Geita.
Discussion
Reader comments
0 contributions