Na Ibrahim Rojala - Geita.
Diwani wa Kata ya Mgusu Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Yohana Buhabi amekabidhi Kompyuta 43 kwa Shule ya Sekondari Mgusu hatua inayotarajiwa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika ufundishaji na ujifunzaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, wakati wa makabidhiano ya kompyuta hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amewataka Walimu na Wanafunzi kuzitumia kompyuta hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuongeza ufanisi wa elimu.

‘Mheshimiwa mkuu wa mkoa ameelekeza waalimu na wanafunzi wa shule hii hakikisheni kwanza mnavitumia vifaa hivi kwa makusudi na malengo ambayo mheshimiwa diwani ametoa,isiwepo tena leo tunaviona viko hapa, kesho tunaviona viko mahala kwingine kwaajili ya matumizi ambayo hayakukusudiwa,’ ameeleza Myenzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Riziki Marco, amesema Mbunge Chacha Wambura ameunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia meza za kuweka kompyuta kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo.

‘Mheshimiwa Mbunge wa Geita mjini anawaomba uongozi na wanafunzi wa shule ya Sekondari Mgusu pamoja na wanafunzi wote,vifaa hivi au kompyuta hizi zimepatikana kwahiyo tuzilinde na tuzitumie vizuri ili ziweze kufaa kizazi cha darasa hili lililopo na darasa lijalo,’ amesema Riziki.
Baadhi ya walimu na wanafunzi wameeleza kuwa msaada huo utarahisisha ufundishaji, ujifunzaji na kuongeza uelewa wa matumizi ya teknolojia shuleni.


Discussion
Reader comments
0 contributions