Na Daniel Gahu - Katavi.
Kufuatia matumizi ya teknolojia ya TEHAMA katika idara mbalimbali za Serikali mkoani Katavi, mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mkoa, Joseph Mkumbwa amesema mkoa wa Katavi umepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ambapo kwa sasa hakuna sekta ya serikali inayofanya kazi bila kutumia TEHAMA kutokana na mchango wake katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema katika kuimarisha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa, serikali imeendelea kuweka miundombinu bora ikiwemo mitandao ya simu na redio ili kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa kwa wakati.

Mkoa wa Katavi unatumia mifumo mbalimbali ya kidigitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hatua ambayo imesaidia kurahisisha utendaji kazi, kuongeza uwajibikaji pamoja na kuimarisha usalama wa taarifa.
“Mifumo hiyo imeundwa kuendana na uhitaji wa wananchi na taasisi mbalimbali, hivyo imeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” amesema Mkumbwa.

Aidha, amesema mkoa una mikakati ya kuhakikisha Katavi inakuwa mkoa wa kidigitali kwa kutumia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano ya mtandaoni ikiwemo WhatsApp, Instagram, Facebook, YouTube, X pamoja na tovuti ya mkoa ya https://katavi.go.tz/ kwa lengo la kuwafikishia wananchi taarifa muhimu kwa haraka zaidi.

Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi hususan vijana kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya TEHAMA na kuitumia vizuri ili kujiongezea kipato kutokana na uhitaji mkubwa wa teknolojia hiyo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa sasa.
Discussion
Reader comments
0 contributions