Na Ibrahim Rojala - Geita.
Licha ya mchango mkubwa wa punda katika shughuli za kiuchumi na usafirishaji kwa jamii, bado wanyama hao wanaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kubebeshwa mizigo mizito kupita uwezo wao, matumizi ya mikokoteni isiyo salama, vipigo vinavyosababisha majeraha pamoja na magonjwa mbalimbali kama pepopunda na matatizo ya mfumo wa hewa.
Hayo yameelezwa Juni 24, 2025 na Afisa Elimu Ustawi wa Wanyama ambaye pia ni Afisa Mifugo kutoka Shirika la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA), Diana Msemo, wakati wa ziara ya kufuatilia matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Ustawi wa Punda katika Kata ya Magenge, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, mradi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya ASPA na Brooke East Africa.

“Changamoto tuliyoikuta hapa ni punda kuwa na vidonda vingi ambavyo vinasababishwa na mikokoteni mizito isiyo na vifaa kazi maalum kwaajili ya wanyama,lakini pia kuna changamoto hiyo hiyo ya vidonda kutokana na changamoto ya kuchapwa au kuongozwa bila mbinu sahihi za uongozaji wa punda”amesema Diana
Ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kubadili mitazamo juu ya punda ikiwa ni pamoja na kuwajengea uelewa juu ya uwepo wa sheria,kanuni na kujengewa hali ya utu wa kuzingatia kuwa punda ni mnyama anayeweza kufanya kazi bila kupigwa,asiye na madhara yoyote na mwenye kustahimili hali zote.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mratibu wa Mradi wa Ustawi wa Punda kwa Mkoa wa Geita kutoka ASPA, Phares Mabija, amesema baadhi ya waswaga punda bado wanatumia mikokoteni isiyokuwa rafiki kwa wanyama hao. Hali hiyo imechochea juhudi za kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wasafirishaji kuhusu matumizi sahihi ya mikokoteni pamoja na matunzo bora ya punda.
“Tumekuja Magenge kwasababu tunataka kubadilisha tabia na mitazamo ya waswaga punda wa hapa maana waswaga punda wa hapa wamekuwa wakitumia material ambayo si salama kwa mnyama punda,wapo wanaotumia mikokoteni ambayo si salama kwa punda,” ameeleza Mabija.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Kata ya Magenge na msimamizi wa vikundi vya wanyama kazi, George Sebastian Mahudi, amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo kumekuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa uelewa wa wafugaji kuhusu ustawi wa punda, hali iliyochangia kuboresha afya zao na kuongeza uzalishaji.
“Kwa namna ilivyo ngumu kumtunza mnyama punda mpaka akapata mtoto,ni juhudi kubwa zimefanyika kwa bwana Jumanne, ukimpumzisha punda ndio anaweza kupata ile tabia yake ya asili ya kupata watoto,” amebainisha George.

Mfugaji wa punda, Joseph Robert amesema mafunzo yanayotolewa kupitia mradi huo yamechangia kuimarika kwa afya za punda wao na kuwahamasisha kuunda kikundi cha wafugaji wa punda katika kata ya magenge iliyo na vikundi viwili kwa alengo la kubadilishana uzoefu na kuboresha ufugaji.
Naye Mfugaji, Jumanne Sokoine amesema mradi huo umemsaidia kuelewa umuhimu wa kuwapumzisha punda, kuwapatia matibabu kwa wakati na kuzingatia sheria za ustawi wa wanyama, jambo lililochangia punda wake kuwa na afya bora na kuongezeka kwa uzazi.



Discussion
Reader comments
0 contributions