Wananchi wa manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuunda vikundi vya ujasiriamali na kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na mikopo yenye riba kubwa inayowadidimiza kimaendeleo.
Hayo yamesemwa na Meya wa manispaa ya Kahama Mh Kaniki Mataluma katika mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Nyasubi akieleza kuwa mikopo yenye riba kubwa imekuwa kikwazo cha maendeleo, hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mataluma amesema aliwahi kusimamia kikundi kimoja cha vijana ili kiweze kupata mkopo na kujikwamua kiuchumi, lakini wakati wa ukaguzi wa shughuli zao wanakikundi walitoweka na kutokomea kusikojulikana.

Amesema tukio hilo lilimfedhesha sana na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa waaminifu na kutumia mikopo wanayopewa kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Fedha hizi tumekuwa tukizitoa kwa vikundi vya ujasiriamali vinavyoomba na kukidhi vigezo. Hivyo nawasihi wananchi muunde vikundi na muwe na miradi yenye tija ili mpate fedha hizo na kuongeza mitaji yenu" Amesema Kaniki.
Mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Suzan Paschal amesema yeye ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri na kwamba mkopo huo umemsaidia kuondokana na utegemezi kwa mume wake.
Amesema awali alikuwa akichukua mikopo yenye riba kubwa kutoka kwa wakopeshaji wa mitaani, hali iliyomfanya kutumia sehemu kubwa ya mapato ya biashara kulipa madeni badala ya kukuza mtaji na kuimarisha maisha yake.

Suzan amewashauri wananchi wengine kuacha kutegemea mikopo yenye riba kubwa na badala yake kuunda vikundi vya ujasiriamali ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri.
“Mimi ni miongoni mwa wanafaika wa mikopo ya halmashauri,imenisaidia sana kutokuwa tegemezi kwa mume wangu,niwashauri wanawake wenzangu achene mikopo ya Kausha damu chukueni mikopo halmashauri ambayo haina riba kubwa” Amesema Suzan.
Discussion
Reader comments
0 contributions