Jeshi la Anga la Marekani limeondoa na kuzirudisha nyumbani ndege zake zote za kivita zilizokuwa zikitumiwa kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kutoka katika kituo cha kijeshi cha RAF Fairford kilichopo nchini Uingereza.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia uchunguzi wa mpango wa shambulio la kigaidi lililolenga kituo hicho cha jeshi, pamoja na melengo mengine ya mifumo shirikishi ya ulinzi kati ya nchi hizo mbili.

Ndege hizo za mashambulizi ya angani zimerudishwa katika vituo vyake vya awali nchini Marekani.
Taarifa hiyo ni kulingana na afisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) aliyezungumza siku ya Jumapili kwa sharti la kutobainishwa jina kutokana na kile alichoeleza unyeti wa taarifa za kijeshi.

Wataalamu na wafuatiliaji wa usafiri wa anga, ikiwa ni pamoja na muungano wa Military Air Tracking Alliance, wameeleza kuwa walishuhudia lundo la ndege za kivita aina ya B-52 na B-1 zikiendesha operesheni zake kutokea katika kituo hicho cha RAF Fairford tangu mwanzoni mwa vita dhidi ya Iran.

Hatua hii imejiri huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiendelea kutathmini kile ameita machaguo sahihi kuhusu vita dhidi ya Iran ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufanya mashambulizi mapya ingawa hapo awali aliwaahidi raia wa Marekani kwamba oparesheni hiyo ingechukua wiki chache tu.
"Nina maamuzi ya kufanya kuhusu Iran. Iran imesambaratishwa vibaya sana. Kwa hiyo swali pekee lililobaki ni kwamba itakuwa kwa njia nyepesi, au kwa njia ngumu," alieleza Rais Trump alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi wakati akiondoka White House kuelekea kwenye mkutano wa hadhara nchini Ohio.
Discussion
Reader comments
0 contributions