Hatua kali imechukuliwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika Manispaa ya Singida, baada ya kubainika kwa tabia ya baadhi ya wananchi na wafanyabiashara ya kutupa taka katikati ya barabara mara tu baada ya magari ya usafi kupita, hali inayohatarisha usafi na maandalizi ya msimu wa mvua za El Niño.
Agizo hilo la marufuku limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, wakati wa ziara ya kukagua vikundi vya kijamii vya CBRM vinavyohusika na matengenezo ya kawaida ya barabara chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe
Gondwe amesema amekuwa akishuhudia taka zikiwekwa katikati ya barabara baada ya magari ya kuzichukua kupita, akisisitiza kuwa tabia hiyo si sahihi na inapaswa kukomeshwa mara moja.
Amewataka wafanyabiashara na wananchi kutumia mapipa ya kuhifadhia taka hadi magari yatakapofika kuzichukua.
“Ni marufuku kuweka uchafu katikati ya barabara, hasa maeneo ya mjini, kwa sababu hakuna utaratibu wa magari kuja kuchukua taka katikati ya barabara. Elimu imeshatolewa, hivyo wataalamu wa mazingira na afya wachukue hatua mara moja,” alisema Gondwe.
Aidha, Gondwe amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji kuwafahamisha wananchi ratiba za ukusanyaji taka ili wajue muda unaofaa kuzitoa.
Amesisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira katika maandalizi ya msimu wa mvua za El Niño.
Kwa upande wa programu ya CBRM katika Manispaa ya Singida, imetengewa Sh milioni 191.25. Hadi sasa, vikundi 10 vimewezeshwa kutekeleza matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 50.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe
Discussion
Reader comments
0 contributions