Na Adam Msafiri - Mara.
Wakazi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wilayani Bunda, mkoani Mara, wameiomba Serikali kuharakisha hatua za kudhibiti wanyamapori waharibifu na wakali, wakisema mashambulizi ya tembo yameendelea kusababisha uharibifu wa mazao, hasara za kiuchumi na kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza katika kongamano la utoaji elimu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na fursa za mikopo kwa wananchi wa vijiji vinavyozunguka Pori la Akiba la Ikorongo, wananchi hao wamesema licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali, bado changamoto ya Tembo na wanyamapori wengine waharibifu imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo yao.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa mara nyingi hulazimika kulinda mashamba yao usiku kucha ili kuyakinga dhidi ya tembo, hali inayowahatarisha na wakati mwingine kusababisha majeraha au vifo wanapojaribu kukabiliana na wanyama hao.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wanapokutana na wanyamapori, ikieleza kuwa tembo wamekuwa na mabadiliko ya kitabia yanayowafanya kuwa hatari zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Maafisa wa TAWA wamesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona wanyamapori wameingia kwenye makazi au mashamba badala ya kujaribu kukabiliana nao wenyewe, hatua ambayo inaweza kuhatarisha maisha yao.
Wakati huo huo, wabunge wa Mkoa wa Mara wamewataka wananchi kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na wataalamu wa uhifadhi kuhusu namna salama ya kukabiliana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, huku wakiitaka Serikali kuendelea kuimarisha mikakati ya kupunguza athari zinazowakabili wananchi waishio pembezoni mwa maeneo ya hifadhi.

Vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Ikorongo vimekuwa vikikabiliwa mara kwa mara na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hususan Tembo, hali ambayo imeendelea kuathiri shughuli za kilimo na ustawi wa wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions