Skip to main content

MAN CITY HATARINI KUSHUSHWA DARAJA

Klabu ya soka ya Manchester City inakabiliwa na kesi ya ukiukaji wa kanuni za fedha inayohusisha mashtaka 115 ambayo yanatikisa ulimwengu wa kandanda.

MAN CITY HATARINI KUSHUSHWA DARAJA
Studio Narration JAMBO FM

MAN CITY HATARINI KUSHUSHWA DARAJA

0:00 --:--

Klabu ya soka ya Manchester City inakabiliwa na kesi ya ukiukaji wa kanuni za fedha inayohusisha mashtaka 115 ambayo yanatikisa ulimwengu wa kandanda.

Chanzo cha sakata hilo kinarejea mwaka 2008 wakati kundi la Abu Dhabi United Group chini ya Sheikh Klabu ya Manchester City imejikuta katikati ya moja ya sakata kubwa zaidi kuwahi kutokea Mansour lilipoinunua Manchester City.

Ndani ya muda mfupi, klabu hiyo ilibadilika kutoka timu ya kawaida ya Ligi Kuu na kuwa moja ya vilabu vyenye nguvu zaidi duniani,mafanikio ambayo yalikuja sambamba na matumizi makubwa ya fedha katika usajili wa wachezaji, jambo lililoibua maswali kutoka kwa wapinzani na wachambuzi kuhusu namna klabu hiyo ilivyokuwa ikifadhili ukuaji wake wa haraka.

Mwaka 2018, hali ilibadilika baada ya jarida la Kijerumani la Der Spiegel kuchapisha nyaraka za ndani za klabu zilizovuja zilizodai kuonesha uwepo wa taarifa zisizo sahihi za kifedha, mikataba ya udhamini yenye utata na mbinu mbalimbali zilizodaiwa kutumika kuficha hali halisi ya mapato ya klabu ambapo Manchester City ilikataa madai hayo na kusisitiza kuwa nyaraka hizo zilipatikana kinyume cha sheria pamoja na kutafsiriwa nje ya muktadha wake.

Baada ya uchunguzi wa miaka kadhaa, Ligi Kuu ya England Februari 2023 ilitangaza kuwa imewasilisha mashtaka 115 dhidi ya Manchester City yanayohusisha kipindi cha kati ya mwaka 2009 na 2018 na kujumuisha madai ya kutotoa taarifa sahihi za kifedha, ukiukaji wa kanuni za faida na uendelevu, ukiukaji wa kanuni za Financial Fair Play pamoja na kushindwa kushirikiana kikamilifu na wachunguzi wa Ligi.

Kesi hiyo ilisikilizwa kwa faragha kati ya Septemba na Desemba mwaka 2024 mbele ya tume huru,tangu wakati huo wadau wa soka duniani wamekuwa wakisubiri kwa hamu matokeo yake kutokana na uzito wa mashtaka yanayoikabili klabu hiyo hata hivyo, hadi sasa hakuna hukumu iliyotolewa rasmi kwa umma, jambo ambalo limeendelea kuongeza sintofahamu na mjadala mkubwa katika dunia ya mpira wa miguu.

Kinachofanya kesi hii kuwa ya kipekee ni ukubwa wa athari zake Manchester City imekuwa moja ya vilabu vilivyotawala soka la England katika kipindi kinachochunguzwa, ikitwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu na kujijengea hadhi ya nguvu mpya katika kandanda ya Ulaya.

Endapo madai dhidi yake yatathibitishwa rasmi, kesi hii inaweza kubadili namna historia ya mafanikio ya klabu hiyo itakavyotazamwa katika miaka ijayo.

Manchester City imeendelea kusisitiza kuwa haina hatia na ina ushahidi wa kutosha kujitetea huku Uongozi wa klabu ukionesha kujiamini tangu mwanzo wa mchakato huo na umeeleza mara kadhaa kuwa unaamini ukweli utaibuka mwisho wa kesi.

Iwapo hukumu hiyo itatangazwa rasmi, hatua inayofuata itakuwa kusikiliza hoja kuhusu adhabu zinazoweza kutolewa na Kanuni za Ligi Kuu ya England zinatoa nafasi ya hatua mbalimbali za kinidhamu ikiwemo faini, kupunguzwa pointi au adhabu nyingine za kimashindano.

Hata hivyo, hakuna adhabu yeyote iliyothibitishwa hadi sasa na suala hilo litaamuliwa katika hatua zinazofuata za mchakato wa kisheria.

Wakati mashabiki wa Manchester City wakisubiri kwa wasiwasi, wapinzani wao nao wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya kesi hiyo ambayo wengi wanaiona kuwa mtihani mkubwa kwa uadilifu wa mfumo wa usimamizi wa fedha katika soka la kisasa, bila kujali matokeo ya mwisho yatakuwa yapi, sakata la mashtaka 115 tayari limeingia katika Historia kama moja ya kesi kubwa na zenye mvuto mkubwa kuwahi kuikumba Ligi Kuu ya England.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.