Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kushirikiana na Serikali katika kutunza na kuhudumia vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza badala ya kutegemea wahisani kutoka nje kwani mambo hayo yamepitwa na wakati.
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Juni 21, 2026 katika harambee ya uchangiaji wa jengo la kitega uchumi cha Kanisa la Anglikana jijini Dodoma.

Amesema, “mambo ya misaada yamepitwa na wakati na hata katika bajeti Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusisitiza kuwa na bajeti ya nchi ambayo inategemea rasilimali za ndani ya nchi.”
Dkt. Mwigulu pia ametoa rai halmashauri zote nchini ziandae orodha ya vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza na kuona namna ya kuvisaidia ambapo amesisitiza si vema kuwaandikia watu hao barua za kwenda kuomba misaada pindi wanapofika kwenye ofisi za umma.

Waziri Mkuu amesema awali katika maeneo mbalimbali nchini ilizoeleka kuwa vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu viliendeshwa kupitia misaada kutoka nje ya nchi dhana ambayo watu wanatakiwa kuachana nayo.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahimiza Watanzania kuendelea kusimama katika mafundisho mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa dini ikiwemo kuendeleza amani na umoja wa kitaifa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kuendeleza mradi wa ujenzi wa kitega uchumi kwa sababu ukuaji wa uchumi ni miongoni mwa malengo muhimu ya maendeleo.
Awali, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Kasisi Canon Dkt. George Lawi alisema ili kuimarisha uwezo wa kifedha na kupunguza utegemezi, Kanisa la Anglikana Tanzania lilianzisha mradi wa kitega uchumi jijini Dodoma na kuhakikisha linakuwa na vyanzo endelevu vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa majukumu ya kiroho na kijamii kwa ufanisi zaidi.

Alisema jengo hilo linatarajiwa kutoa huduma mbalimbali zikiwezo za hoteli, ofisi na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa kanisa na Taifa kwa ujumla.

Discussion
Reader comments
0 contributions