Hakuna kitu kizuri kwenye mahusiano kama kujua mwenzako anapenda nini. Unapomjua mwenzako anachokipenda, inakusaidia katika suala zima la kudumisha uhusiano wenu.
Unapomfanyia yale anayoyapenda si kwamba atafurahi tu bali pia unamtengenezea kumbukumbu nzuri na unajenga nafasi ya pekee katika maisha yake. Unamfanya aone umuhimu wako, atambue utu wako na akupe thamani ya kuwa mwenzi wake wa maisha. Ule ubinadamu na mambo mazuri unayomfanyia mwenzi wako ndiyo silaha yako ya kumfanya azidi kukupenda.
Pia unajiweka katika nafasi nzuri ya mwenza wako kukupa thamani kama ile ambayo wewe unampa na kukufanyia mema kama au zaidi ya yale ambayo umekuwa ukimfanyia. Ndio maana leo nimekuja na mada hii, mambo ambayo wanaume wanapenda kuyasikia kutoka kwa wenza wao.
KUHITAJI MSAADA
Kwa uhalisia mwanaume anapenda kujihisi kuwa anahitajika, hivyo mwanamke anapomuambia anahitaji msaada wake, anajisikia amani na faraja kwa sababu anaona kwamba ana nafasi muhimu katika maisha ya mwenza wake.
Anajua ni wajibu wake kumsaidia mwanamke wake, hivyo unapokuwa na mwenzi wako, onyesha kwamba unamhitaji na unahitaji akusaidie katika baadhi ya mambo yako.
Mathalan, unashindwa kuweka balbu; unapomuambia, “Baby, naomba unisaidie kuweka hii balbu,” hakika hujisikia vizuri kwa sababu umeonyesha kwamba unathamini uwezo na msaada wake.
Mtaalamu wa saikolojia ya mapenzi, Tiya Cunningham-Sumter, anasema: “Mwanaume anapenda kuona anahitajika kumsaidia mwenza wake hata kwa yale mambo madogomadogo.”

KUSIFIWA
Kwa kawaida wanaume wengi wanapenda kusifiwa, hususani na wenza wao. Mwanamke anapomwona mwanaume wake akifanya jambo fulani, hasa lile la kumsaidia, ni muhimu kutambua juhudi hiyo na kumwonyesha kwamba umeiona na kuithamini.
Mwanamke anapomsifia mwanaume wake, huwa anajisikia faraja na kujiamini zaidi kwa sababu anatambua kwamba juhudi zake hazipiti bila kuonekana.
Msifie mwanaume wako kwa kazi nzuri aliyofanya; maneno hayo yanaweza kuongeza sana chachu ya mapenzi na kumfanya azidi kuwa na hamasa ya kukufurahisha.
Mshauri wa mambo ya mapenzi, Carolyn Cole, amewahi kusema: “Mwanaume anapenda kusifiwa kwa ujuzi, hivyo mfanye ajue kwamba unatambua kwamba ni mzuri katika jambo fulani.”

KUONEKANA MKAMILIFU
Mwanaume anapenda kuonekana amekamilika kwa kila kitu mbele ya mwanamke anayempenda.
Unapomweleza kwamba amekamilika, kwamba hakuna kitu ambacho atahitaji na ushindwe kukutimizia, inampa nguvu sana mwanaume na kumfanya ajione ana nafasi ya pekee katika maisha yako.
Pale unapoona amekamilika kama mwanaume katika kila idara, mfanye ajue. Mwambie kwa lugha ya kimahaba kwamba unamkubali, unamthamini na kwamba amekamilika kwako. Hiyo inaweza kumpa imani zaidi na kumfanya ajione ana thamani kubwa kwako.
Mwanaume anapojisikia anakubalika na kuthaminiwa na mwanamke anayempenda, hali hiyo inaweza kuimarisha zaidi ukaribu na uhusiano wao. Atazidi kuona umuhimu wa nafasi yake katika maisha yako na kuthamini zaidi upendo unaompa.

KUHESHIMIKA
Mwanaume anapenda sana kuona anaheshimika na mwanamke wake. Hivyo, mwonyeshe kwamba unamheshimu, mwonyeshe kwamba unamthamini na unatambua mchango wake katika maisha yako.
Heshima ni sehemu muhimu katika uhusiano kwa sababu humfanya mwenza ajione ana thamani na nafasi katika maisha ya mwenzake.
Unapomfanyia hivyo mwanaume, unamfanya ajione kwamba uwepo wake una maana kwako na kwamba unathamini kile anachokifanya katika uhusiano wenu.
Ni muhimu kumwonyesha heshima si wakati wa furaha pekee, bali pia katika nyakati ambazo mnapitia changamoto. Unapomthamini, kumheshimu na kutambua mchango wake, unajenga mazingira mazuri ya kuimarisha uhusiano na kumfanya akuone kuwa una thamani kubwa maishani mwake.

Kumjua mwenza wako na kufahamu mambo anayoyapenda ni sehemu muhimu ya kujenga uhusiano wenye upendo na maelewano.
Wakati mwingine mwanaume hahitaji mambo makubwa sana ili ajisikie anapendwa; anaweza kuhitaji tu kusikia maneno machache kutoka kwa mwanamke anayempenda na kuona kwamba juhudi zake zinatambuliwa.
Kumwonyesha kwamba unamhitaji, kumsifia, kumweleza kwamba anakukosha, kumfanya ajue kwamba unamwona amekamilika na kumheshimu kunaweza kumfanya ajisikie ana nafasi muhimu katika maisha yako.
Hata hivyo, maneno hayo yanapokuwa ya kweli na kuambatana na vitendo, huwa na maana kubwa zaidi. Kwa sababu katika uhusiano, si suala la kusema tu “nakupenda,” ila ni kujua namna ya kumfanya mtu unayempenda ajisikie kwamba anapendwa, anaheshimiwa na anathaminiwa.
Discussion
Reader comments
0 contributions