Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ametoa agizo kwa mkandarasi anayejenga Chuo cha Umahiri wa Michezo Malya kuhakikisha awamu ya kwanza ya mradi huo inakamilika kabla ya Aprili 2027.
Agizo hilo amelitoa Oktoba 13, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku 2 Wilayani Kwimba, akiwa amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ukaguzi na uzinduzi wa miradi 14 ya maendeleo.

Makonda ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 32 unajumuisha ujenzi wa hosteli za wanafunzi, Akademia ya michezo na mabwawa ya kisasa ya kuogelea, hatua ambayo itakifanya chuo hicho kuwa cha kwanza na cha pekee kwa umahiri wa michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema uwekezaji huo ni fursa kubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho cha vijana na watoto wenye vipaji vya michezo nchini.

Akizungumza na wananchi, Waziri Makonda amesisitiza kuwa kukamilika kwa chuo hicho kutafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Kwimba, ikiwemo ajira na ujenzi wa miundombinu ya ziada.
Amewaomba wananchi kukiona kituo hicho kama chachu ya maendeleo ya eneo hilo, na sio mradi wa kawaida.
"Mtakuwa na viwanja vya nyasi pamoja na jukwaa la kubeba watu 2000 hadi 2500, wananchi wa eneo hili wanufaike, kukiwa na mechi kali wacheze hapo.
Nawaomba kituo hiki kiwe chachu ya maendeleo na watoto wetu wakue wakijua kuna mradi wa thamani hapa kwao na una thamani ya bilioni 32,"
Discussion
Reader comments
0 contributions