Na Daniel Gahu - Katavi.
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imeendelea kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani kwa kuwaandaa makarani 77 wa mapato kupitia semina elekezi iliyolenga kuwajengea uwezo kabla ya kuanza rasmi majukumu yao katika vituo mbalimbali vya ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri hiyo.
Semina hiyo imelenga kuhakikisha kuwa watendaji hao wanaelewa kwa kina wajibu wao, sheria, kanuni na taratibu za ukusanyaji wa mapato ya umma, sambamba na matumizi sahihi ya mifumo ya kisasa ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Emmanuel Mgaya, amesema mafanikio ya halmashauri katika ukusanyaji wa mapato yanategemea kwa kiasi kikubwa uadilifu na uwajibikaji wa makarani hao watakapokuwa kazini.
Mgaya amesisitiza kuwa makusanyo yote ya mapato lazima yafanyike kupitia mfumo wa kielektroniki wa POS, huku akiwataka makarani kuhakikisha kila muamala unasajiliwa kwenye mfumo huo bila kukiuka taratibu zilizowekwa.

Ameongeza kuwa fedha zote zitakazokusanywa zinapaswa kuwasilishwa benki kwa wakati kama ilivyoelekezwa, hatua ambayo itasaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha za umma.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Clavery Reginald, amewakumbusha makarani hao kuwa wao ni watumishi wa umma, hivyo wanapaswa kuzingatia maadili ya utumishi katika kila hatua ya utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema nidhamu ya kazi, utii wa sheria na kanuni za utumishi, uvaaji wa mavazi rasmi pamoja na kuwahudumia wananchi kwa heshima na weledi ni mambo yatakayowajengea imani wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
Reginald amesisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa uaminifu, kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya halmashauri pamoja na kulinda maslahi ya serikali wakati wote.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Otman Kasmya, amewapongeza makarani hao kwa kuaminiwa na kupewa jukumu muhimu la kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Amesema nafasi waliyopewa si ya kawaida, bali ni dhamana kubwa inayohitaji uwajibikaji, uzalendo na uadilifu wa hali ya juu katika kuhakikisha kila mapato yanayostahili yanakusanywa kwa mujibu wa sheria.

Kasmya amewataka makarani hao kuhakikisha wanawahi katika vituo vyao vya kazi, kuepuka utoro, kufanya kazi kwa bidii na kutoa taarifa mapema wanapokutana na changamoto zozote ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
"Tunawapeleka kwenye mageti sio mkawe mapambo, tunawataka mkasimamie kikamilifu ukusanyaji wa mapato, kubaini na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato, pamoja na kukagua mizigo ipasavyo," amesisitiza Kasmya.

Katika semina hiyo, makarani hao pia wamepewa elimu kuhusu matumizi salama ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato, ambapo wameonywa kutoshiriki vitendo vya ukiukwaji wa sheria kama vile kutumia akaunti au majina ya watumiaji (username) ya wenzao kuingia kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato.
Viongozi wa halmashauri wameeleza kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai na kinaweza kusababisha hatua kali za kinidhamu pamoja na hatua za kisheria dhidi ya mhusika.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imeweka wazi kuwa itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa makarani hao ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zote za ukusanyaji wa mapato zinafuatwa kikamilifu, huku ikilenga kuongeza mapato ya ndani yatakayowezesha kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo kwa wananchi.
Semina hiyo ni sehemu ya mkakati wa halmashauri kuimarisha usimamizi wa mapato ya serikali, kuongeza uwajibikaji wa watendaji na kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Wilaya ya Tanganyika.
Discussion
Reader comments
0 contributions