Na Ibrahim Rojala, Chato - Geita.
Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajiwa kuwasili wilayani Chato mkoani Geita Mei 28, 2026 kwa ajili ya kushiriki shughuli za mazishi ya Mama mzazi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, Mama Suzana Ngolo Mussa ambaye anatarajiwa kuzikwa Mei 29, 2026 katika makaburi ya familia.
Akizungumza na vyombo vya habari Mei 28, 2026 nyumbani kwa Hayati Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema Makamu wa Rais anamuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mazishi hayo.

‘Maandalizi yote yamekamilika,tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameshiriki kikamilifu katika mazishi haya kwa kuhakikisha kwamba gaharama kama nilivyosema mwanzo zinabebwa na serikali kwa kuhakikisha mama yetu tunamuenzi na kumpumzisha katika nyumba yake ya milele’ameeleza Shigela
Aidha, RC Shigela ameeleza kwamba viongozi mbalimbali wa kitaifa wanatarajiwa kuhudhuria, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira pamoja na viongozi wastaafu akiwemo Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa.

Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe amesema wananchi wa jimbo hilo wameishi kwa ukaribu na marehemu, na kumpoteza kwake ni pigo kubwa kwa jamii.
‘Wananchi wengi wa Chato walimfahamu huyu mama toka mwanae Magufuli akiwa mbunge wa Jimbo hili mwaka 1995, kwahiyo watu wengi na wananchi wengi walikuwa wanashiriki katika shughuli mbalimbali kwenye familia,na yeye mama alikuwa mtu mcheshi,alikuwa anapokea kila aina ya mtu aliyekuwa anakuja hapa’ameeleza Magembe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila ameuelezea msibahuo kuwa na taswira ya kitaifa kutokana na Mama huyo(Suzana Ngolo Mussa) ndiye aliyezaa na kumlea kiongozi wa nchi kwa kutambua mchango wake katika malezi,usimamizi hadi kumuwezesha hayati Dkt,John PombeMagufuli kuwa Rais wa nchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions