Na Ibrahim Rojala - Geita.
Inakadiriwa kuwa mkoa wa Geita una watu wapatao 95,000 wanaoishi na mambukizi ya Virusi vya Ukimwi na asilimia 80 kati yao wametambua hali zao za maambukizi ya virusi hivyo.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Dkt. Omari Sukari ameleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku Afya ya Jamii ya Geita mwaka 2026 yaliyoambatana na matembezi ya afya, uchangiaji damu na kuwaaga wawakilishi wa mkoa wa Geita wanaotarajiwa kwenda kupanda mlima kilimanjaro, ili kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kupitia kampeni ya Kili Challenge 2026 inayoendeshwa kwa ufadhili wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML).
Akizungumza kuhusu mchango wa Kili Challenge katika makabiliano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi mkoani Geita, Dkt.Sukari ameushukuru mgodi wa dhahabu wa Geita GGML kwani kupitia kampeni hiyo, mkoa ulipata Shilingi Milioni 100, zilizotumika katika utoaji wa elimu, upimaji wa VVU katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Wilaya ya Geita.

“Wataalam wa afya wamepata nafasi ya kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali na kwakweli wamefanya kazi kubwa, tunawapongeza lakini tunawashukuru sana GGML,” ameeleza Dkt. Sukari
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML), Duan Campbell ameshukuru ushiriki wa wadau mbalimbali, waliofanikisha kufanyika kwa maadhimisho ya siku hiyo akieleza kwamba ili kujenga jamii imara na yenye afya ni lazima kushirikiana na kufanya mipango kwa pamoja.

“Pamoja na kwamba GGML inachimba lakini madini inapenda kuwa na mipango endelevu ambayo inaimarisha mafanikio ya jamii ya Geita Kwa maana ya kwamba initiatives mbalimbali tunazozifanya kama hii ziweze kubadilisha maisha ya wakazi na wananchi wa Geita ili jamii iweze kuwa bora zaidi kuliko namna iliyokuw mwanzo,” ameeleza Duan.
Aidha amesema kampeni kupanda mlima Kilimanjaro kwa miguu na waendesha baiskeli inafanywa kwa ushirikiano na Serikali kupitia TACAIDS na kueleza kuwa washiriki hawauawakilishi mgodi wa GGML pekee bali jamii nzima ya wana Geita na Tanzania nzima kwa ujumla.

Naye Meneja wa Mfuko wa GGML Kili Trust Challenge, Stephen Mhando ameeleza kwamba washiriki wa Kili Challenge 2026 wanatarajiwa kuuwakilisha mkoa wa Geita katika zoezi la kuupanda mlima Kilimanjaro kuanzia Julai 24 hadi 30 mwaka huu na kuongeza kuwa kupitia kampeni ya Kili Challenge 2026 iliyozinduliwa Juni 30,2026 jijini Dar Es Salaam,GGML imelenga kuchangisha kiasi cha shilingi bilioni 2.6 zitakazotumika katika afua za mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA), Leticia Moris amewataka vijana mkoani Geita pamoja na Taifa kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na Magonjwa yasiyokuwa yakuambukiza sambamba na Ukimwi.

“Lakini Kwanini nasema hivyo, Mimi ni ‘role model’, nimeweza kutambua afya yangu mwaka 1997 lakini ukitambua afya yako mapema ukigundulika una maambukizi ukaanza tiba yako mapema unaweza kuishi maisha marefu sana kama wengine,” ameeleza.
Nahodha Msaidizi wa waendesha baiskeli wanaotarajiwa kushiriki Kili Challenge 2026,Thomas Shimba amesema matarajio yake ni kuwa washiriki wa wapya wa mwaka huu watafanikiwa kuumaliza mzuguko vizuri kutoka na mazoezi yaliyofanyika ndani ya kipindi cha miezi mitatu mfululizo wakati mshiriki Mwantumu Fereji,amesema anaamini ushiriki wake utachangiamapambano dhirdi ya virusi vya ukimwi nchini wakati.

Kupitia hotuba ya kilele cha siku hiyo, Katibu Tawala wa halmashauri ya wilaya ya Geita,Lucy Beda amesema kuendeleza utoaji wa elimu sahihi,uhamasishaji wa upimaji,mwendelezo wa mapambano dhidi ya unyanyapaa vimetajwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Aidha ameupongeza mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) kwa kuwezesha maadhimisho ya siku hiyo na kuwezesha timu ya Kili Chalenge 2026 ambapo kupitia zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.6 zinatarajiwa kuchangishwa,akieleza kwamba ushirikiano kati ya serikali,sekta binafsi,wataalam wa afya na jamii ni muhimu sana katika kujenga Jamii yenye afya na yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS ni mpango wa kuhamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, kupitia GGML Kili Trust, rasilimali hukusanywa na kuelekezwa kwenye miradi inayonufaisha moja kwa moja watu wanaoishi na VVU pamoja na taasisi zinazowahudumia.

Ndani ya mwaka huu, Kili Trust imeendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na asasi za kiraia kutoka maeneo mbalimbali nchini zinazotekeleza programu za kusaidia watu walioathiriwa na VVU na UKIMWI, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kufikia watu wengi zaidi.
Aidha tangu kuanzishwa mwaka 2002, mpango huu umeendelea kuleta watu binafsi, taasisi na washirika pamoja kuchangia jitihada za kinga, tiba, matunzo na msaada kwa jamii.
Discussion
Reader comments
0 contributions