Na Adam Msafiri - Mara.
Zaidi ya majiko banifu 300 yamegawiwa kwa wananchi wa vijiji vya kata ya Gwitiryo wilayani Tarime mkoani Mara, katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kupunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya za wananchi dhidi ya athari za matumizi ya nishati chafu.
Mradi huo unaotajwa kuwa mkombozi kwa wanawake na familia nyingi za vijijini, umeendelea kuleta matumaini mapya kwa wakazi wa kata ya Gwitiryo ambapo wananchi wameanza kunufaika na majiko yanayotumia nishati kwa ufanisi zaidi huku yakipunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa majiko hayo, Diwani wa kata ya Gwitiryo Issaya Sangai maarufu Tobiko, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi yenye kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini.
Aidha, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Gwitiryo Majubo Gamaha amesema mradi huo utasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake Meneja wa usambazaji wa majiko banifu kutoka kampuni ya Geita Millennium Star Limited Hamisi Cashirila, amesema matumizi ya majiko hayo yana mchango mkubwa katika kupunguza ukataji holela wa miti, kuhifadhi mazingira pamoja na kupunguza madhara ya kiafya yanayosababishwa na moshi wa kuni na mkaa.
Amesema hatua hiyo pia inaunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi na salama zaidi.

Baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo akiwemo Angelina Joseph pamoja na Pius Mang’era wa kijiji cha Kitagasembe, wameeleza kuwa majiko hayo yatawasaidia kupunguza gharama za matumizi ya mkaa, kuni na gesi, kuokoa muda wa kupika pamoja na kuboresha afya za familia zao kutokana na kupungua kwa moshi majumbani.

Wananchi hao pia wameiomba serikali kuendelea kupeleka miradi kama hiyo katika maeneo mengine ya vijijini ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Discussion
Reader comments
0 contributions