Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, amewataka vijana wanaonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, kudumisha umoja na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwapa fursa wanufaika wengine.
Mahundi aliyasema hayo, alipofanya ziara katika Kata ya Rubafu, Wilaya ya Bukoba, na kukagua mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unaotekelezwa na vikundi vya vijana vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

Akizungumza na wanakikundi hao, alisema utoaji wa mikopo hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeyaagiza mamlaka za serikali za mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Bi. Fatina Laay, kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha vikundi vinapata mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

Mahundi aliwasisitiza vijana hao kuendelea kudumisha mshikamano na ushirikiano ndani ya vikundi vyao, akibainisha kuwa baadhi ya vikundi huonyesha umoja wakati wa kupata mikopo lakini huanza kutofautiana pindi miradi inapoanza kuleta faida.
"Pale mnapopata fedha mnakuwa wamoja, lakini wakati wa mavuno wengine huanza kutengana. Endeleeni kushikamana ili miradi yenu iwe endelevu na ilete manufaa yaliyokusudiwa," alisema.

Pia aliwataka kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha mzunguko wa fedha na kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo wa serikali.
Katika mradi huo, Kikundi cha Kishenge chenye vijana saba kilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 27, huku Kikundi cha Mchumia Jua chenye vijana watano kikipokea mkopo wa kiasi Cha shilingi milioni 27 nacho, na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kufikia shilingi milioni 54.

Kila kikundi kinafuga samaki 35,000 kwa njia ya vizimba, na kinatarajiwa kuvuna takribani tani 13 za samaki, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wanakikundi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Ziara ya Mahundi ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera, ambapo pia alitembelea Makao ya Wazee Kilima pamoja na Kituo cha Ntoma kinachohudumia watoto yatima wenye umri wa kuanzia kuzaliwa hadi miaka miwili.
Discussion
Reader comments
0 contributions