Na Ibrahim Rojala - Geita.
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Geita umefanikiwa kukamata jumla ya magari 12,638 yaliyopimwa katika mizani ya Bwanga na Chato mkoani Geita yakiwa yamezidisha uzito.
Idadi hiyo ya magari yaliyokamatwa kwa kosa la kuzidisha uzito ni sawa na asilimia 21.2 ya magari 59,574 yaliyopimwa kuanzia mwezi Disemba, 2025 hadi Julai, 2026 katika mizani iliyopo mkoani Geita.
Aidha, kati ya hayo, jumla ya magari 44 ambayo ni sawa na asilimia 0.1 yalikutwa na kosa la kuzidisha uzito wa zaidi ya asilimia 5 inayoruhusiwa kisheria na kutozwa faini ya Milioni 5.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Geita, Mhandisi Hosea Machaka ametoa taarifa hiyo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika ofisi za mkuu wa mkoa mjini Geita,amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa TANROADS kusimamia zoezi la kudhibiti uzito wa magari barabarani kwa kutumia mizani na kupunguza uharibifu wa barabara.

Amesema, ukaguzi wa hali ya barabara uliofanyika Mei, 2026 umebainisha asilimia 48.54 ya barabara zote zina hali nzuri, asilimia 50.17 zina hali ya wastani na asilimia 1.95 zina hali mbaya.
“Katika mwaka wa fedha 2025/26 TANROADS mkoa wa Geita ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 12.309 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara na madaraja.
“Jumla ya mikataba 46 ya kazi za matengenezo ya barabara, madaraja yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.523 ilitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2025/26”, amesema Mhandisi Hosea
Amebainisha kuwa hadi kufikia Julai, 2026 jumla ya fedha zilizopokelewa ni Shilingi Bilioni 1.209 sawa na asilimia 9.8 ya bajeti ya matengenezo ya Shilingi Bilioni 12.309.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27 TANROADS mkoa wa Geita imetengewa jumla ya sh bilioni 15.195 kutekeleza kazi za matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara na madaraja.
Aidha ameeleza kuwa hadi kufikia Julai 27, 2026 jumla ya zabuni 22 zenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 7.72 sawa na asilimia 50.8 ya bajeti ya matengenezo zipo katika hatua ya manunuzi katika mkoa wa Geita ambao una mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa km 1,019.13 zinazohudumiwa na Wakala ya Barabara (TANROADS).
Discussion
Reader comments
0 contributions