Skip to main content

MAENDELEO SEKTA YA KILIMO: WAZIRI MKUU AIPA TANO TADB

Na Gideon Gregory - Dodoma.

MAENDELEO SEKTA YA KILIMO: WAZIRI MKUU AIPA TANO TADB

Na Gideon Gregory - Dodoma.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, huku akiitaka kuongeza uwezo wa kifedha ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi kupitia huduma za mikopo yenye tija.

Akizungumza leo Agosti 1,2026 baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, Waziri Mkuu amesema benki hiyo imeendelea kuwa chachu ya mageuzi ya kilimo kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji inayochochea uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya sekta ya kilimo, lakini mafanikio ya muda mrefu yanahitaji taasisi imara za kifedha kama TADB ambazo zitahakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mitaji kwa urahisi bila kutegemea ruzuku pekee.

"Tunahitaji TADB yenye mtaji mkubwa zaidi ili iweze kukidhi mahitaji ya sekta ya kilimo, kufadhili ununuzi wa pembejeo, mbolea, mashine za kisasa pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao. Hii ndiyo njia ya kujenga kilimo chenye tija na ushindani," amesema Waziri Mkuu.

Aidha, ameielekeza TADB kuimarisha ushirikiano na Wizara za Kilimo, Mifugo pamoja na TAMISEMI katika kuwekeza kwenye miundombinu ya baada ya mavuno, ikiwemo ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi mazao ili kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kufadhili miradi ya kimkakati inayobadili taswira ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Amesema hadi sasa TADB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya kufadhili miradi ya umwagiliaji, huku ikiendelea kusaidia uzalishaji wa mazao ya biashara ikiwemo kahawa kupitia vyama vya ushirika katika mikoa ya Kagera na Kigoma.

Nyabundege amesema banda la TADB limevutia idadi kubwa ya wadau waliotaka kupata taarifa kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo, huku wengi wakionesha nia ya kushirikiana katika miradi ya kuongeza tija ya uzalishaji.

Ameongeza kuwa TADB pia imewezesha uwekezaji wa mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo, unaotumia teknolojia kutoka Misri na wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi, hatua inayochochea uzalishaji, kulinda mazingira na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.

Kwa mujibu wa Nyabundege, uwekezaji huo umeanza kuleta matokeo chanya kwa kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuzalisha ajira kwa Watanzania na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Maonesho ya Nanenane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha mafanikio, ubunifu na fursa mbalimbali zinazolenga kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo ndiyo mhimili mkuu wa uchumi wa Tanzania.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.