Na Saulo Stephen – Singida.
Madiwani wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa ya Singida, wametakiwa kuandaa programu maalumu za kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupunguza matumizi ya nishati za jadi.
Wito huo umetolewa na Afisa Misitu na Mazingira Mkoa wa Singida, Charles Kidua, wakati akizungumza na madiwani katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Manispaa ya Singida.

Kidua amesema madiwani wana nafasi kubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuwahamasisha wananchi, hususan wanaoishi vijijini, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kufanikisha kampeni ya Serikali ya “Kumtua Mama Kuni”, ambayo inalenga kupunguza mzigo kwa wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta kuni pamoja na kuboresha afya na mazingira.
Kwa mujibu wa Kidua, matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kupunguza athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, sambamba na kupunguza uharibifu wa mazingira unaochangiwa na ukataji wa miti.

Amewataka madiwani kutumia nafasi zao kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kutoa elimu ya kutosha kuhusu faida za nishati safi, ili kuongeza uelewa na kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati katika jamii.
Warsha hiyo fupi ya kuwajengea uwezo madiwani imehudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa lengo la kuwapa uelewa zaidi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na namna ya kuwafikia wananchi.
Mpango huo wa utoaji elimu unatarajiwa kuendelea katika wilaya zote za Mkoa wa Singida, huku madiwani wakitarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Discussion
Reader comments
0 contributions