Na Adam Msafiri - Musoma.
Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, limeibua mvutano mkali baada ya kuhoji uhalali wa wajasiriamali kuendelea kufanya biashara katika eneo la hifadhi ya barabara ya Majita Road, wakidai hatua hiyo ni kinyume cha sheria na inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
Hoja hiyo imeibuliwa katika kikao cha robo ya mwisho cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Musoma kilichokuwa kikijadili mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
Baadhi ya madiwani wameeleza kutoridhishwa na kurejea kwa wafanyabiashara katika eneo hilo, wakisema awali waliondolewa kwa sababu za usalama na kuhifadhi miundombinu ya barabara, lakini sasa wameanza tena kufanya shughuli zao bila maelezo ya wazi.

Diwani wa Viti Maalumu, Naima Minga, ni miongoni mwa madiwani waliotilia shaka uhalali wa biashara hizo kuendelea kufanyika ndani ya eneo la hifadhi ya barabara.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mshikamano, Njofu Katama, amesema kuruhusu biashara katika eneo hilo ni kwenda kinyume na sheria pamoja na kuweka maisha ya watumiaji wa barabara katika hatari.
Naye Diwani wa Viti Maalumu, Amina Masisa, amesisitiza kuwa ni muhimu mamlaka za manispaa kufuata taratibu na kuhakikisha maeneo ya biashara yanakuwa salama kwa wananchi wote.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao Majita Road wamedai kuwa kurejea kwao kulitokana na maelekezo waliyopewa na viongozi wa manispaa, huku wakieleza kuwa biashara hizo ndizo tegemeo lao kuu la maisha.
Akizungumzia suala hilo, Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Nyabiti, amesema manispaa itaendelea kutafuta suluhisho litakalolinda usalama wa wananchi huku likizingatia pia ustawi wa wafanyabiashara.
Mvutano huo unatajwa kuchangiwa na maamuzi ya baadhi ya watendaji wa manispaa kuruhusu shughuli za biashara kuendelea katika eneo hilo kwa lengo la kuongeza mapato ya halmashauri, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa madiwani na wananchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions