Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imewaomba madiwani kujiunga na mpango wa “TAKUKURU Rafiki” unaolenga kuzuia vitendo vya rushwa katika jamii kupitia mazungumzo, ushirikiano na utatuzi wa kero kabla hazijawa kubwa.
Wito huo umetolewa katika semina fupi iliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa wa Kagera iliyowakutanisha madiwani, watendaji pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa lengo la kujadili uwajibikaji na wajibu wa viongozi katika kuzuia rushwa.

Akizungumza katika semina hiyo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Leonard Swai alisema mpango wa TAKUKURU Rafiki unalenga kuhakikisha changamoto zinazojitokeza kwenye miradi ya maendeleo zinatatuliwa mapema kupitia mazungumzo badala ya kusubiri hatua za mwisho za utekelezaji wa miradi.
Alisema mara nyingi malalamiko kuhusu miradi hutolewa baada ya miradi kufikia hatua za mwisho, jambo ambalo husababisha ugumu katika kurekebisha changamoto zilizojitokeza.

“Tusisubiri mpaka watu wakamatwe na kwenda mahakamani, huko kuna sheria ngumu. Ni vizuri tukawa timu na kushirikiana kutatua changamoto mapema. Wananchi wengi wanaofika TAKUKURU wanakuwa wamepitia kero ambazo hazijapatiwa majibu. Ushirikiano kati ya madiwani, wakuu wa idara na watendaji utaepusha changamoto nyingi na kusaidia kulinda miradi ya maendeleo,” alisema Swai.
Aidha, aliwataka madiwani kuendelea kusimamia watendaji pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba katika suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza ufanisi wa halmashauri hiyo. Pia aliwaonya watendaji kuacha matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato ili kuepuka hatua za kisheria.

Nao, baadhi ya madiwani walieleza kuwa semina hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu masuala ya rushwa na umuhimu wa kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya maendeleo ili waweze kubaini na kutoa taarifa za viashiria vya rushwa mapema kwa njia rafiki na kusaidia miradi kukamilika kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Hussein Laay alisema mpango wa TAKUKURU Rafiki ni muhimu kwa kuwa unasaidia kuchambua changamoto na kubaini ni zipi zinahitaji hatua za kisheria na zipi zinaweza kutatuliwa kwa mazungumzo.

Aliishukuru TAKUKURU kwa kutoa mafunzo hayo kwa madiwani akisema wao ni wasimamizi wakuu wa maendeleo katika kata zao, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya rushwa.
Discussion
Reader comments
0 contributions