Na Daniel Gahu - Katavi.
Mwenezi wa Vijana wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Taifa, Elizabeth Kasera, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Maalum ya Taifa kupitia Jukwaa la Vijana la chama hicho, ametoa ufafanuzi kuhusu sakata lililoibuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana wa CHAUMMA Mkoa wa Katavi, Elizabeth Sigera.
Kwa mujibu wa Kasera, Sigera alinukuliwa akitoa tuhuma dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, huku akijitambulisha kama mwanachama wa CHADEMA, jambo ambalo Kasera amesema si la kweli kwa kuwa Sigera alikuwa mwanachama wa CHAUMMA.
Kasera amesema kitendo hicho ni kinyume na maadili ya chama na hakikubaliki. Ameeleza kuwa kutokana na hatua hiyo, CHAUMMA kimeamua kumvua Elizabeth Sigera uanachama pamoja na nyadhifa zote alizokuwa akizishikilia ndani ya chama.

"Kitendo alichokifanya Elizabeth Sigera ni kiovu na kisichovumilika. Chama kimeamua kumfuta uanachama na kumvua rasmi vyeo vyote alivyokuwa navyo ndani ya CHAUMMA," amesema Kasera.
Kasera amesisitiza kuwa CHAUMMA, kama chama cha upinzani, kinatambua CHADEMA kuwa ni miongoni mwa vyama vikuu vya upinzani nchini. Hivyo, amesema si sahihi kwa wanachama wa CHAUMMA kushambulia vyama vingine vya upinzani badala ya kushirikiana katika malengo yao ya kisiasa.
"Sisi vyama vya upinzani adui yetu mkubwa ni CCM. Hivyo si vyema sisi kwa sisi kushambuliana," amesema.
Aidha, Kasera amesema chama kinaamini kila mtu anapaswa kuwajibika kwa matendo yake binafsi, na kwamba makosa yanayodaiwa kufanywa na Sigera hayapaswi kubebwa na taasisi ya CHAUMMA.
"Makosa aliyoyafanya Elizabeth Sigera atayabeba yeye mwenyewe, si taasisi. Kuna watu wanaendekeza njaa, ndiyo maana wanatumika vibaya," ameongeza.
Kasera amesema ameamua kutoa ufafanuzi huo baada ya kupokea simu nyingi kutoka kwa wananchi waliotaka kujua msimamo wa chama kuhusu sakata hilo.
Ameeleza kuwa baadhi ya watu walichanganya majina yake na ya Elizabeth Sigera kutokana na wote kuitwa Elizabeth, jambo lililosababisha sintofahamu iliyohitaji kuwekwa wazi.
Discussion
Reader comments
0 contributions