Skip to main content

MABORESHO SHERIA ZA USAJILI CAF KUZINUFAISHA SIMBA, YANGA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya maboresho makubwa katika kanuni za usajili kwa klabu zinazoshiriki michuano yake mikubwa ya klabu, ikiwemo CAF Champions League na CAF Confederation Cup.

MABORESHO SHERIA ZA USAJILI CAF KUZINUFAISHA SIMBA, YANGA
Studio Narration JAMBO FM

MABORESHO SHERIA ZA USAJILI CAF KUZINUFAISHA SIMBA, YANGA

0:00 --:--

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya maboresho makubwa katika kanuni za usajili kwa klabu zinazoshiriki michuano yake mikubwa ya klabu, ikiwemo CAF Champions League na CAF Confederation Cup.

Hatua hiyo, inayolenga kuongeza ushindani, kupunguza athari za uchovu na majeraha kwa wachezaji pamoja na kuongeza ubora wa michuano hiyo katika ngazi ya kimataifa.

Miongoni mwa mabadiliko makubwa ni ongezeko la idadi ya wachezaji ambao klabu inaweza kuwasajili katika mashindano hayo, ambapo sasa kila klabu inaruhusiwa kuwa na kikosi cha hadi wachezaji 40 badala ya 30 waliokuwa wakiruhusiwa awali.

CAF imechukua hatua hiyo kwa kuzingatia ratiba yenye msongamano wa mechi na mahitaji ya klabu kuwa na kikosi kipana kinachoweza kutoa nafasi kwa makocha kufanya mzunguko wa wachezaji bila kupunguza ushindani wa timu.

Kwa upande wa mabadiliko wakati wa mchezo, CAF imeifanya rasmi kanuni ya kuruhusu kila timu kufanya mabadiliko matano ndani ya dakika 90 za mchezo.

Sambamba na hilo, idadi ya wachezaji wanaoweza kukaa kwenye benchi la akiba imeongezwa kutoka saba hadi tisa, jambo linalowapa makocha nafasi kubwa zaidi ya kuwa na chaguo la wachezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya mchezo, majeraha au uchovu.

Mabadiliko mengine muhimu yanahusu dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.

Klabu sasa zinaruhusiwa kuongeza hadi wachezaji wapya wanne katika kikosi chake wakati wa dirisha hilo.

Hata hivyo, mchezaji anayesajiliwa katika kipindi hicho anatakiwa kuwa hajawahi kucheza mechi yoyote ya mashindano ya CAF msimu huo akiwa na klabu nyingine.

Sheria hii inalenga kuzuia matumizi yasiyo na uwiano ya wachezaji huku ikiendelea kutoa nafasi kwa klabu kuimarisha vikosi vyake katikati ya msimu.

Katika hatua nyingine kubwa, CAF imeondoa kizuizi kilichokuwa kikimzuia mchezaji kuchezea klabu mbili tofauti katika msimu mmoja wa mashindano yake.

Chini ya utaratibu mpya, mchezaji aliyewahi kusajiliwa na kucheza hatua za awali za mashindano akiwa na klabu moja anaweza kuhamia klabu nyingine na kusajiliwa upya katika mashindano hayo msimu huohuo, ikiwa taratibu zote za uhamisho na usajili zitakuwa zimekamilishwa.

Mabadiliko haya yanaondoa kwa kiasi kikubwa dhana ya mchezaji kuwa cup tied, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikimzuia mchezaji kuendelea na mashindano baada ya kuhama klabu.

CAF pia imeweka utaratibu mpya wa madirisha manne ya usajili kwa klabu zinazoshiriki mashindano hayo.

Usajili wa hatua za awali unafanyika kuanzia Agosti 1 hadi 15, huku usajili wa raundi za mchujo ukiwa kati ya Agosti 16 na Septemba 30.

Kwa hatua ya makundi, klabu zitakuwa na nafasi ya kusajili wachezaji kuanzia Oktoba 1 hadi 31, wakati dirisha la mwisho litakuwa kati ya Januari 1 na 31 kwa ajili ya kufanya marekebisho ya vikosi kabla ya hatua za mtoano.

Pamoja na madirisha hayo, CAF imeweka pia sharti la muda kwa usajili wa wachezaji wapya.

Mchezaji mpya anatakiwa kuwa amesajiliwa kikamilifu kwenye mfumo wa CAF angalau saa 72 kabla ya kuanza kwa mchezo husika, ili aweze kuruhusiwa kushiriki.

Kanuni hii inalenga kuhakikisha kuwa taarifa za wachezaji zinakamilishwa mapema na kuzuia changamoto za kiutawala zinazoweza kujitokeza muda mfupi kabla ya mechi.

Kwa ujumla, maboresho hayo yanaashiria mwelekeo mpya wa CAF katika kuifanya michuano ya klabu Afrika kuwa na mfumo unaoweza kuendana na mahitaji ya kisasa ya soka.

Maboresho hayo pia yanatoa nafasi kwa klabu kuwa na vikosi vipana, kufanya usimamizi bora wa wachezaji na kukabiliana na ratiba yenye msongamano wa mashindano ya ndani na kimataifa.

Mabadiliko hayo, pia yanaweza kuwa na athari kubwa kwa klabu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya CAF hususani Simba na Yanga, kwa kuwa zitakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kupanga vikosi vyao kulingana na ratiba na kufanya maboresho wakati wa msimu.

Kuongezeka kwa idadi ya wachezaji hadi 40 na kuruhusiwa kwa mchezaji kuchezea klabu nyingine katika msimu huohuo kunaweza pia kuongeza ushindani katika usajili na kufanya dirisha la Januari kuwa muhimu zaidi kwa klabu zinazolenga kufika mbali katika mashindano ya Afrika.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.