Madereva wa Mabasi yaendayo Mikoani Mkoani Katavi wameonywa dhidi ya matumizi ya simu, vilevi na kuendesha kwa mwendo usio salama, huku abiria wakitakiwa kuwa sehemu ya kwanza kutoa taarifa wanapoona dalili za dereva kuhatarisha maisha ya watu ndani ya basi.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Katavi, Leopold Fungu, wakati wa ukaguzi wa magari ya abiria uliofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Mizengo Pinda, ukihusisha maafisa wa usalama barabarani kutoka Mikoa ya Katavi na Rukwa.
Fungu amesema madereva wamekabidhiwa dhamana kubwa ya kubeba uhai wa abiria, hivyo matumizi ya simu wakati wa kuendesha, pombe au vilevi vingine pamoja na uzembe wa aina yeyote vinaweza kuhatarisha maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja.
Amesema tabia ya baadhi ya madereva kuchepuka barabarani na kushindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ni miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha ajali, hivyo amewataka madereva kuhakikisha usalama unakuwa kipaumbele kabla ya kuanza safari.
Katika ukaguzi huo magari 22 ya abiria yalikaguliwa, ambapo manne yalibainika kuwa na hitilafu ndogo ndogo na kuagizwa kufanyiwa marekebisho kabla ya kuendelea na safari, hatua inayolenga kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Chabruma Gama amesema ukaguzi huo ni sehemu ya operesheni ya pamoja katika Kanda namba moja inayojumuisha Mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Kigoma.
Chabruma amesema abiria nao wana nafasi muhimu katika kuzuia ajali kwa kutoa taarifa kwenye maeneo ya ukaguzi endapo watabaini dereva anaendesha kwa mwendo kasi, ametumia pombe au anaonesha dalili za kuhatarisha usalama wa safari.
Katika zoezi hilo, madereva pia walifanyiwa vipimo vya kubaini viashiria vya matumizi ya vilevi, hususani pombe huku hatua hiyo ikiibua ujumbe muhimu kwamba usalama wa safari hauishii kwa dereva pekee,abiria na vyombo vya usalama wote wana nafasi ya kuzuia ajali kabla haijatokea.
Discussion
Reader comments
0 contributions