Na Saulo Stephen - Singida.
Katika maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, Mkoa wa Singida umeendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotarajiwa kuzinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa jiwe la msingi wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Katika ziara hiyo ambayo imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Singida kwa lengo la kuhakikisha miradi yote inakidhi viwango vya ubora, thamani ya fedha na mahitaji ya wananchi.

Ukaguzi huo umefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, ukianzia katika eneo la Soko la Mnada la Bukundi Mkoa wa Simiyu, ambalo linatarajiwa kutumika kukabidhia Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Singida.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na mradi wa sekta binafsi wa ujenzi wa nyumba ya kulala wageni katika eneo la Ibaga, mradi wa maji Kata ya Msingi, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Malaja unaotekelezwa kwa mapato ya ndani na nguvu za wananchi, pamoja na mradi wa vijana wa kikundi cha Tuamke Vijana Group wa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti uliopo Ndurumo.

Kamati hiyo pia ilikagua ujenzi wa daraja la kivuko katika Kijiji cha Iyelembo, mradi wa wananchi wa ujenzi wa barabara kuelekea Shule ya Msingi Mnolo unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi pamoja na Mradi wa Kituo cha Afya Iguguno.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, RC Dendego amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa miradi, usafi wa mazingira na utekelezaji wa miradi inayokidhi viwango vinavyostahili kwa kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya maendeleo na uwakilishi wa Serikali kwa wananchi.

Pia amewapongeza wananchi wa Mkalama kwa kujitolea kuboresha miundombinu katika maeneo yao na vijana walioanzisha viwanda vidogo hususan vya uchakataji wa alizeti.
Aidha, amehimiza uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa ili kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Singida na kufikia azma ya kuwa kitovu cha viwanda na biashara. Vilevile amewataka vijana kutumia kikamilifu fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili kuanzisha miradi yenye tija, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa.

Discussion
Reader comments
0 contributions