Na Gideon Gregory - Dodoma.
Rais Samia Suluhu Hassan amefunga rasmi Wiki ya Maonesho ya Kilimo na Mifugo, huku akitoa maagizo matatu kwa Wizara na taasisi husika, ili kuboresha sekta hizo.
Katika maagizo hayo, Rais Samia amezitaka Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
"Naagiza Wizara hizi kwa kushirikiana na Tamisemi mkashughulikie kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, najua imepungua kiasi lakini bado ipo, haiwezekani tukawa na magomvi badala ya kuzalisha mali," amesema Samia.
Katika hatua nyingine Rais Samia ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa juhudi za kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata mikopo na mitaji ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.

Pia ameelekeza kuwa upatikanaji wa fedha kwa wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Kakurwa, amesema kutokana na ongezeko la bajeti,wizara hiyo imefanikiwa kutekeleza jukumu lake la kuongezeka idadi na thamani ya mifugo nchini.
Dkt. Bashiru amesema kuwa thamani ya mifugo imeongezeka kutoka takribani Shilingi trilioni 26 kwa mwaka 2020/2021, hadi kufikia takribani Shilingi trilioni 33 kwa mwaka 2024/2025 kwa makundi yote ya mifugo.
Katika hotuba yake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Frank Nyabundege amemweleza Rais kuwa benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 1.55 kwa miradi 862, huku Sh trilioni 1.32, sawa na asilimia 84, zikitolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Kwa mujibu wa TADB, mikopo hiyo imewanufaisha zaidi ya Watanzania milioni 2.6 katika mikoa yote 31 ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mkurugenzi huyo amesema fedha hizo pia zimewezesha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, maghala, vihenge na viwanda vya uchakataji, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko.
“Fedha hizi zimefika mashambani, kwenye miradi ya mifugo na uvuvi, zimejenga mifumo ya umwagiliaji, maghala, vihenge na viwanda vya uchakataji, na hivyo kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko,” amesema.
Discussion
Reader comments
0 contributions