Na Saulo Stephen - Singida.
Katika kuadhimisha wiki ya maziwa duniani, Maafisa kutoka Bodi ya maziwa Tanzania wametembelea Mkoa wa Singida kwa lengo la kufuatilia na kuboresha maendeleo ya sekta ya maziwa nchini.
Kupitia ziara hizo, viongozi na wataalamu wa Bodi hiyo wamekutana na wafugaji, wasindikaji wa maziwa, wafanyabiashara pamoja na vikundi vya ushirika ili kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutoa elimu kuhusu uzalishaji bora wa maziwa, usafi, lishe ya mifugo na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Awali,Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt.Fatuma Mganga akizungumza na wataalamu hao ofisini kwake aliwaasa kuhakikisha wanatumia muda wao mwingi katika kuhakikisha wanasimamia wazalishaji wa maziwa hayo kuyavuna kwa wingi kwa kuwafundisha namna sahihi ya uzalishaji na usindikaji wake kwa kiwango kikubwa na sio kwa matumizi madogo ya nyumbani pekee.
Amesema kuwa ili kufikia lengo la kuhakikisha kila mmoja anakunywa maziwa ya kutosha yapaswa kuwa na wazalishaji wengi jambo ambalo halina uhalisia kwani wafugaji wengi wamekua wakifuga mifugo mingi huku wakizalisha kiwango kidogo cha maziwa ambacho hakitoshi kwa jamii.

Ziara hiyo pia imesaidia kukagua ubora wa maziwa yanayozalishwa na kuhakikisha sheria na kanuni za sekta ya maziwa zinafuatwa.
Aidha, Bodi ilitumia ziara hiyo kuhamasisha uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuimarisha soko la bidhaa za maziwa kwa manufaa ya wafugaji na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Discussion
Reader comments
0 contributions