Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ameulalamikia upande wa Jamhuri kuwa unachelewesha mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili kwa kufungua maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufani na kusema ucheleweshwaji huo kuna mtu atalipa.
Lissu ametoa lalamiko hilo hii leo Agosti 10, 2026 baada ya kuanza kwa kesi hiyo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Amesema, “leo majaji ni siku ya 166 tangu tarehe 24 Februari 2026, wamekwenda Mahakama ya rufaa nimewashinda lakini tumerudi baada ya kupotezeana siku 166. Tuendelee lakini itapofika siku itabidi tuzungumze hii kesi ya bure na huu ucheleweshaji wa bure uliofanywa na Mawakili na anayewatuma someone has to pay for this.”
Hata hivyo, Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga umekanusha madai hayo na kusema Mkurugenzi wa Mashtaka hana nia ya kuchelewesha kesi, bali kilichotokea ni upande huo kutekeleza haki yake ya kisheria ya kuomba marejeo ya shauri Mahakama ya Rufani, baada ya kuhisi kuwa kuna sehemu Majaji hawakuamua kwa usahihi.
“Haikuwa nia ya upande wa Jamhuri kuchelewesha kesi. Kuhusu kushinda na kushindwa, kushindwa kwa Wakili mwenye weledi ni jambo la kawaida,” alisema Katuga.
Discussion
Reader comments
0 contributions