Mchezaji wa timu ya taifa ya Ureno Raphael Leão, amepewa jezi namba 7 ambayo awali ilikuwa ikivaliwa na mchezaji mwenzake Cristiano Ronaldo kufuatia Ronaldo kuondoka kwenye kikosi cha Ureno kuelekea mchezo dhidi ya Denmark. Leão ambaye kwa kawaida huvaa namba 17 akiwa na taifa hilo sasa atavaa namba 7 iliyobeba historia kubwa ya Ronaldo katika soka la kimataifa.
Kwa Ronaldo namba 7 haikuwa namba ya kawaida ilihusishwa naye kwa karibu tangu alipokuwa akiendelea kujenga jina lake katika soka la kimataifa na hatimaye ikawa sehemu ya chapa maarufu ya CR7. Akiwa ndani ya jezi hiyo Ronaldo aliandika historia kubwa akiwa na Ureno, akiongoza timu hiyo kwenye mafanikio makubwa na kuweka rekodi nyingi za kimataifa. Ndiyo maana picha ya mchezaji mwingine kuivaa namba hiyo inaonekana kama ishara ya mabadiliko ya kizazi ndani ya timu ya taifa.

Leão sasa amekabidhiwa jukumu hilo, ingawa kwa muktadha wa sasa hii ni zaidi ya mabadiliko ya namba kwenye orodha ya wachezaji. Kanuni za UEFA Nations League zinataka wachezaji walio kwenye kikosi cha mchezo wapewe namba kuanzia 1 hadi 23. Ronaldo alipokuwa nje ya kikosi cha mchezo dhidi ya Denmark nafasi ya namba 7 ilihitaji kupewa mchezaji mwingine ndipo Leão akapewa namba hiyo na Fábio Silva kuchukua namba 17 aliyokuwa akiivaa Leão.
Hapa ndipo simulizi ya Ureno inapokutana na iile ya Argentina wakati Ureno imempa mchezaji mwingine jezi ambayo imekuwa ikitambulishwa na Ronaldo Argentina imekuwa ikikabiliwa na mjadala kuhusu mustakabali wa namba 10 baada ya Lionel Messi. Messi ameifanya namba hiyo kuwa sehemu kubwa ya utambulisho wake akiwa na Argentina, na baada ya mwisho wa safari yake ya kimataifa, kumekuwa na mjadala kuhusu kama namba hiyo inapaswa kuendelea kutumika au kustaafishwa. Hata hivyo, kustaafisha kabisa namba hiyo katika mashindano ya FIFA kuna vikwazo vya kanuni hivyo si jambo lililofanyika rasmi.
Tofauti kubwa ni kwamba kwa Ronaldo, namba 7 tayari imeonekana mgongoni mwa kizazi kinachofuata. Leão amevaa namba hiyo na hivyo kutoa picha ya moja kwa moja ya namna jezi inaweza kuendelea kutumika hata baada ya mchezaji aliyeifanya kuwa maarufu kutokuwepo. Kwa Messi mjadala umejikita zaidi kwenye namna ya kuheshimu namba 10 ambayo imebeba urithi wake mkubwa lakini jezi yenyewe bado ni sehemu ya mfumo wa namba unaotumika na timu ya taifa ya Argentina. FIFA, kwa mfano ilimtaja Messi akiwa namba 10 kwenye kikosi cha Argentina cha Kombe la Dunia 2026.

Raphael Leão kuvaa jezi namba 7 haimaanishi kama atakuwa Cristiano Ronaldo mpya lakini ni mwanzo wa ukurasa mwingine wa jezi ambayo tayari imetengenezewa historia kubwa. Ronaldo ameacha alama yake kwenye namba hiyo kama ambavyo Messi ameacha historia yake kwenye namba 10 ya Argentina. Sasa tofauti ni kwamba Ureno imeonyesha moja kwa moja sura mpya ya namba 7 kupitia Leão huku Argentina ikiendelea kujadili namna bora ya kuutunza urithi wa namba 10 baada ya Messi.
Wachezaji wakubwa huondoka, lakini jezi wanazovaa huendelea kuishi. Kwa sasa namba 7 ya Ureno inaanza kuonekana ikiwa na sura ya Raphael Leão lakini kila itakapokuwa mgongoni mwake kumbukumbu za Cristiano Ronaldo zitaendelea kuwepo kwani jezi ni ileile lakini simulizi inaanza kuandikwa upya.
Discussion
Reader comments
0 contributions