Na Saulo Stephen - Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewataka viongozi, wataalamu na wananchi kuimarisha juhudi za kuzuia majanga kabla hayajatokea badala ya kusubiri kuyakabili baada ya kutokea, akisisitiza kuwa kinga ndiyo njia bora ya kupunguza athari za majanga kwa jamii.
Dendego ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Singida kilicholenga kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kukabiliana na majanga yanayoweza kuathiri mkoa.
Amesema baadhi ya majanga husababishwa na shughuli za kibinadamu zinazokiuka maadili na taratibu za mazingira, hivyo elimu kwa wananchi, matumizi ya lugha rahisi katika utoaji wa taarifa pamoja na ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Katika kikao hicho, Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka Maafisa Afya kuongeza juhudi za kutoa elimu ya kinga kwa wananchi, kuimarisha matangazo ya uhamasishaji na kuhakikisha hatua za tahadhari zinazingatiwa katika maeneo yote.
Aidha, amesisitiza kila halmashauri kuunda na kuendesha Kamati za Maafa ili kuhakikisha mkoa unakuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wowote.
Kwa upande wao, wataalamu wa afya walitoa tahadhari kuhusu ugonjwa wa Ebola na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusana na wagonjwa bila tahadhari pamoja na kutoa taarifa mapema pindi dalili zinapojitokeza.
Kikao hicho pia kiliazimia kuimarisha usafi wa mazingira, kuzibua mitaro ya maji, kutenga bajeti za kukabiliana na majanga katika halmashauri zote na kuendelea kuwaondoa nyuki hatarishi kwa kushirikiana na wataalamu wa nyuki, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Misitu.
Hatua hizo zinalenga kuhakikisha Mkoa wa Singida unaendelea kuwa katika hali ya utayari wa kukabiliana na majanga ya asili, kiafya na yale yanayosababishwa na shughuli za binadamu.
Discussion
Reader comments
0 contributions