Tamasha la michezo lililowashirikisha wanafunzi na walimu kutoka shule mbalimbali za sekondari za Manispaa ya Shinyanga, maarufu kama Kombe la Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, limefana huku washindi wakizawadiwa zawadi mbalimbali.

Tamasha hilo limefanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Old Shinyanga, likihusisha michezo mbalimbali ikiwamo kufukuza kuku, kukimbia na magunia, mbio za mita 100, kuvuta Kamba, kukimbia na mayai kwa kutumia vijiko, pamoja na fainali ya mpira wa miguu kati ya wanafunzi wa kidato cha nne na kidato cha sita wa shule ya Sekondari Old Shinyanga.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa tamasha hilo, Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Manispaa ya Shinyanga Richard Makoye, amesema limewawezesha walimu na wanafunzi kukutana pamoja, kuimarisha afya, kujenga mahusiano na kuongeza ari ya kufanya kazi na kujifunza ili kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.

"Kwanza kabisa tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa maelekezo na kuwezesha sekta ya elimu nchini, na Manispaa ya Shinyanga imeendelea kuwa miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza kwa ufanisi sera za elimu, ikiwamo kushiriki matamasha ya michezo yenye lengo la kukuza taaluma," amesema Makoye.
Pia, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwa kuanzisha na kuendelea kuunga mkono matamasha hayo ya michezo shuleni, ambayo yamekuwa chachu ya ukuzaji wa taaluma.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga wakili Julius Mtatiro, amesema aliahidi kuandaa Tamasha la michezo kwa walimu na wanafunzi, na sasa ahadi hiyo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Amesema tamasha hilo limeimarisha umoja na ushirikiano miongoni mwa walimu, limewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza ari pamoja na mbinu za ufundishaji.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndala Hamisa Magulu, amesema bonanza hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa walimu na wanafunzi, kwa kuwa limeongeza ushirikiano kati ya shule mbalimbali, na kusaidia kupunguza changamoto za afya ya akili.
Mmoja wa wanafunzi Daud Charles wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, amesema michezo hiyo imewasaidia kujenga afya, kuimarisha ushirikiano, na kuongeza morali ya kufanya vizuri katika masomo huku akimuomba mkuu huyo wa wilaya kuendelea kuandaa matamasha kama hayo ili yawajenge kiakili.

Discussion
Reader comments
0 contributions