Skip to main content

KNK CUP 2026: WASIMAMIZI WA MASHINDANO WAPEWA SEMINA

Na Ibrahim Rojala, Bukombe - Geita.

KNK CUP 2026:  WASIMAMIZI WA MASHINDANO  WAPEWA SEMINA

Na Ibrahim Rojala, Bukombe - Geita.

Kamati ya Mashindano ya KNK CUP 2026 imeendesha semina maalumu kwa wasimamizi wa mashindano ngazi ya kata, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha michuano hiyo inaendeshwa kwa weledi, haki na kuzingatia sheria za mpira wa miguu.

Semina hiyo imewakutanisha Watendaji wa Kata, Waheshimiwa Madiwani pamoja na viongozi wa vijana kutoka kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe, ambao watakuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu mashindano katika maeneo yao.

Mbali na mafunzo, kamati ya mashindano imekabidhi vifaa muhimu vitakavyotumika wakati wa michuano hiyo, vikiwemo mipira, jezi, tracksuit, vifaa vya huduma ya kwanza (First Aid Kit) pamoja na miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa mashindano iliyoandaliwa na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bukombe (BUDFA).

Akitoa mada katika semina hiyo, Mratibu wa KNK CUP 2026 ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita, Bosco Mwidadi, amesema kuwa masuala yote ya kiufundi yanayohusu uendeshaji wa mpira wa miguu yako chini ya BUDFA, ambayo imeikabidhi Kamati ya KNK CUP mamlaka ya kusimamia mashindano hayo kwa kushirikiana na Afisa Michezo wa Wilaya pamoja na wadau wengine wa mchezo huo.

Mwidadi amewataka Watendaji wa Kata kutekeleza wajibu wao kama wasimamizi wakuu wa mashindano katika ngazi ya kata kwa kuhakikisha ratiba zinafuatwa, sheria zinazingatiwa na michezo yote inafanyika katika mazingira ya haki na utulivu.

Kwa upande wa Waheshimiwa Madiwani, ameeleza kuwa wamepewa jukumu la kuhamasisha wananchi kushiriki mashindano hayo pamoja na kuchangia kuongeza thamani ya zawadi katika kata zao kulingana na uwezo wao. Aidha, madiwani watakuwa wageni rasmi katika fainali zote za ngazi ya kata na watashiriki kukabidhi zawadi kwa washindi.

Watendaji wa Kata, ambao pia ni wasimamizi wa amani katika maeneo yao, wamehimizwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha michezo yote inafanyika kwa amani bila vitendo vya vurugu.

Akizungumzia suala la huduma ya kwanza, Mwidadi amesema kuwa usalama wa wachezaji umepewa kipaumbele katika KNK CUP 2026.

"Kila kata leo imekabidhiwa boksi la huduma ya kwanza lenye dawa na vifaa muhimu kwa ajili ya kutoa huduma ya awali kwa majeruhi. Pia kila timu imesisitizwa kuwa na vifaa vyake vya huduma ya kwanza," amesema.

Kwa mujibu wa waandaaji, mshindi wa jumla wa KNK CUP 2026 atazawadiwa shilingi milioni tano, seti tatu za jezi, mipira mitatu, medali za dhahabu pamoja na kombe la ubingwa. Mshindi wa pili atapata shilingi milioni tatu, seti mbili za jezi, mipira miwili na medali, huku mshindi wa tatu akijishindia shilingi milioni mbili, seti moja ya jezi na mpira mmoja.

Mjumbe kamati kuu na mjumbe wa kamati ya maadiri na nidhamu wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita na mjumbe wa Kamati ya KNK CUP, Erasto Banunu amewataka Watendaji wa Kata, Madiwani na viongozi wa vijana kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa kuzingatia sheria za mpira wa miguu, maadili, utu na lengo la kuimarisha umoja, upendo na amani miongoni mwa wananchi.

"Naomba niwahakikishie kuwa sitasita kuchukua hatua kali dhidi ya timu au mashabiki watakaokiuka taratibu na sheria za mashindano," amesisitiza.

Naye Katibu wa Mashindano hayo, Mwalimu Dominick Kabalega, amewataka Watendaji wa Kata kushirikiana kikamilifu na Polisi Kata ili kuhakikisha usalama unaimarishwa katika kila mchezo utakaochezwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya KNK CUP ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Salabaga, amewataka vijana wa hamasa katika kata zote kutokuwa chanzo cha migogoro kwa kuepuka upendeleo wa timu na badala yake kuhamasisha ushindani wa kirafiki.

Mashindano ya KNK CUP 2026, yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumapili, Juni 28, 2026, katika Viwanja vya Mwenge Uyovu/Runzewe. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Eng. Paskas Muragili, ambaye pia atashuhudia mechi maalumu ya kirafiki kati ya mashabiki wa Simba SC na Yanga SC itakayofungua rasmi pazia la michuano hiyo itakayoanza rasmi Julai Mosi. 

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.