Kivumbi kimetimka Nchini Kenya baada ya Mwanasiasa machachari wa Upinzani nchini humo Edwin Sifuna kutangazwa rasmi kama mgombea wa nafasi ya Urais uchaguzi wa Mwaka kesho 2027.

Edwin Sifuna mwanasiasa mwenye taaluma ya Sheria (wakili) Nchini Kenya na mkulia chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kinachoongozwa na muungano wa upinzani (Azimio la Umoja) ametangazwa rasmi na Muungano wa kisiasa wa Linda Mwananchi kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hatua hiyo inakuja baada ya kuarifiwa hapo nyuma kuwapo kwa migawanyiko na tofauti za kimitazamo baina ya vyama vya upinzani nchini Kenya.

Katika taarifa ya mapema ya viongozi wa muungano huo baada ya kuketi mezani mwishoni mwa juma, wameeleza kukubaliana kwa pamoja na kwa umoja Katika kutatua kero za kiutawala kile wameita zinazotatiza Taifa la Kenya.
Kadharika Viongozi hao walibainisha kuwa Edwin Sifuna ndiye atakayepeperusha bendera ya muungano huo katika mbiringe za Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Pia katika taarifa ya muungano huo imeeleza kusudi lake la kushirikiana na vyama vingine vya kisiasa vyenye maono yanayolandana katika mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ndani ya Taifa hilo.
Sifuna akizungumza kufuatia kutangazwa kwake amesema anamatumaini makubwa juu ya mustakabali wa muungano huo akisema viongozi wake wako pamoja katika safari ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Sifuna ni mwanasiasa mwenye historia ndefu katika siasa za Kenya, awali alihudumu kama Katibu Mkuu wa chama cha ODM tangu mwaka 2018 hadi katikati ya mwaka 2026 na ndiye Seneta wa Kaunti ya Nairobi kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Historia yake ilianza kuchomoza mnamo mwaka 2013 – 2016 chini ya Muungano wa CORD, Alianza rasmi kujihusisha na siasa za kitaifa za upinzani kama Mjumbe wa Kamati ya Kiufundi na Ushauri (Technical/Advisory Committee Member) katika muungano huo wa upinzani wa Coalition for Reforms and Democracy (CORD).
Mwaka 2016 – 2017 Aliendelea kuhudumu kwenye nafasi ya kiufundi na ushauri ndani ya muungano uliyofahamika kama National Super Alliance (NASA). Na hatimaye Mwaka 2017, aligombea kiti cha Seneta wa Nairobi kwa mara ya kwanza kupitia ODM licha ya kutofua dafu kushinda.

Mnamo Februari 2018, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha ODM kuchukua Nafasi ya Ababu Namwamba, nafasi iliyomfanya kuwa mmoja wa wasemaji na viongozi wakuu wa Upinzani nchini Kenya na Mwaka 2022 alichaguliwa kuwa Seneta wa Nairobi akishika nafasi hiyo hadi sasa huku akiwa Naibu Kiranja wa Wachache (Deputy Minority Whip) katika Bunge la Seneti.
Discussion
Reader comments
0 contributions