Na Tryphone Odace - Kigoma.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji (KIUWASA) imesema zoezi la kuboresha na kudhibiti miundombinu ya maji katika eneo la Bwawa la Katubuka linaendelea likiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji wa KIUWASA, Herman Nguki wakati akizungumza na Jambo Fm katika eneo la Bwawa Katubuka ambapo zoezi la kubadilisha na kuunganisha mabomba lilikuwa linafanyika.

Amesema hapo awali kulikuwa na upotevu mkubwa wa maji kupitia miundombinu ya zamani katika eneo la Bwawa la Katubuka hali iliyokuwa ikiisababishia mamlaka hiyo hasara kubwa.
Nguki ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji. Hata hivyo, amesema maboresho yanayoendelea yataongeza ufanisi wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa uhakika.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji, kupunguza upotevu wa maji na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali hiyo muhimu katika eneo la Bwawa la Katubuka.
Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya maji nchini kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya maji na usafi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa urahisi na kwa uhakika.

Discussion
Reader comments
0 contributions