Skip to main content

KISA MFUMO: WAKULIMA MARA WAOMBA MAREKEBISHO MSIMU WA UNUNUZI ZAO LA TUMBAKU

Na Adam Msafiri - Mara.

KISA MFUMO: WAKULIMA MARA WAOMBA MAREKEBISHO MSIMU WA UNUNUZI ZAO LA TUMBAKU

Na Adam Msafiri - Mara.

Wakulima wa zao la tumbaku katika wilaya za Serengeti na Rorya mkoani Mara wameiomba Serikali kufanya marekebisho ya msimu wa ununuzi wa zao hilo, wakisema mfumo wa sasa unasababisha ucheleweshaji wa mauzo na kuwashawishi baadhi ya wakulima kuuza tumbaku kupitia masoko yasiyo rasmi.

Hoja hiyo, imeibuka katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Vyama Wanachama wa WAMACU unaowakutanisha wadau wa zao la tumbaku kujadili namna ya kuboresha uzalishaji, usimamizi wa zao hilo na kukabiliana na changamoto zinazoathiri sekta hiyo.

Baadhi ya wakulima walioshiriki mkutano huo wamesema kuchelewa kuanza kwa msimu wa ununuzi kunawaweka katika mazingira magumu ya kiuchumi na kuchochea biashara ya magendo.

“Tunaiomba Serikali iangalie upya kalenda ya ununuzi wa tumbaku. Wakulima wanapocheleweshewa soko, wengine hulazimika kuuza kwa wanunuzi wasio rasmi ili kukidhi mahitaji yao ya kifedha,” wameeleza baadhi ya wakulima wakati wa mjadala.

Meneja wa WAMACU, Samweli Gisiboyi, amesema ushirikiano kati ya vyama vya ushirika, Serikali na wakulima ni muhimu ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha zao la tumbaku linaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Mara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia kwa karibu shughuli za wakulima na kuwasaidia kufikia malengo ya uzalishaji yaliyowekwa na Serikali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesisitiza umuhimu wa ushirika imara katika kulinda maslahi ya wakulima na kuongeza tija ya zao hilo.

“Vyama vya ushirika vina wajibu mkubwa wa kuwaunganisha wakulima na kuhakikisha wanapata huduma stahiki pamoja na soko lenye tija,” amesema Gowele.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfan Haule, ametoa onyo kwa wakulima wanaojihusisha na utoroshaji wa tumbaku, akisema Serikali haitawavumilia wale wanaokiuka taratibu za biashara ya zao hilo kwa kuuza katika masoko yasiyo rasmi.

Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya tumbaku mkoani Mara kwa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji, kuimarisha ushirika na kudhibiti biashara haramu inayopunguza mapato ya wakulima na Serikali.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.