Na Ibrahim Rojala - Geita.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Jackline Peter (25), mkazi wa Mji Mdogo wa Katoro, Wilaya na Mkoa wa Geita, kwa tuhuma za kumshambulia kwa kutumia fimbo Rahel Jumanne (22), aliyemtuhumu kumwibia fedha zake.
Kwa mujibu wa taarifa kwa iliyotolewa Agosti 30, 2026 na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita,imeeleza kuwa tukio hilo la kikatili lilitokea Agosti 26, 2026, majira ya saa tano asubuhi, nyumbani kwa mtuhumiwa, Jackline Peter aliyedai kuwa ameibiwa fedha kiasi cha Shilingi 60,000/= zilizokuwa kwenye pochi chumbani kwake na kuanza kumtilia shaka Rahel Jumanne aliyekuwa amemtembelea kwake.

Siku ya tukio, baada ya fedha hizo kudaiwa kupotea, mtuhumiwa alimkamata mwathirika na kuanza kumshambulia kwa fimbo na wakati vitendo hivyo vya ukatili vikiendelea, mfanyakazi wa kazi za ndani wa mtuhumiwa alirekodi tukio hilo kwa kutumia simu ya mtuhumiwa na baadaye mtuhumiwa kusambaza picha mjongeo hiyo kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya Jeshi la Polisi kubaini tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, lilianza ufuatiliaji wa mara moja na kufanikiwa kubaini eneo la tukio, kumtambua mtuhumiwa na kumkamata, ambapo kwasasa anaendelea kuhojiwa.

Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hilo na mara baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka husika za kisheria kwa hatua zaidi.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoani Geita limetoa wito kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi. Tuhuma za uhalifu hazimruhusu mtu mwingine kutoa adhabu mwenyewe, badala yake anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria kwa hatua zaidi.
Discussion
Reader comments
0 contributions