Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Kiongozi wa dini, Nabii Nicolaus Suguye, ametoa msaada wa matofali 3,000 na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Kahama Orphanage Center kilichoopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga ili kuboresha usalama wa watoto hao.
Msaada huo umeenda sambamba na mahitaji mbalimbali ya chakula na usafi, yakiwemo unga, mchele, mafuta ya kupikia, sabuni na maharage, kwa ajili ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kabla ya kuanza mkutano wa Injili katika Manispaa ya Kahama, Nabii Suguye amewataka wadau mbalimbali pamoja na watu wenye uwezo kuwa na moyo wa kuwasaidia watoto hao kwa kutoa misaada kulingana na nafasi na uwezo walio nao.
“Watoto hawa ni wetu sote na nijukumu letu kuwalea,Mungu anapokupa nafasi na uwezo wa kifedha tujitahidi kuwatembelea watoto hawa na kuwapa misaada kwani hawana watu wa kuwasaidia zaidi yetu sisi jamii tunaowazunguka” Amesema Nabii Suguye.

Nabii Suguye ameongeza kuwa pamoja na kutoa misaada, ni muhimu kwa jamii kuwa karibu na watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto yatima na kushirikiana katika kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu.
“Tunapokuwa katika majukumu yetu tutenge muda kuja kuwatembelea watoto hawa na kuwasilimia ili nao wajione kuwa wana nafasi katika jamii kama watoto wengine,tuwe nao karibu mara kwa mara huku tukiamini kuwa ujio wetu hapa ni faraja kwao.” Ameongeza Nabii Suguye.

Awali, msimamizi wa kituo cha Peace Orphanage Center Abubakari Issa amesema kituo hicho kina changamoto kubwa ya kukosa uzio hali inayofanya watoto kudhurika kwa kung’atwa na mbwa pamoja kuibiwa vitu mbalimbali katika kituo hicho zikiwemo nguo.
“Tatizo kubwa katika kituo chetu ni ukosefu wa uzio,mifugo na vitu mbalimbali vya watoto vinaibiwa sana pamoja na watoto kupata matatizo kama kung’atwa na Mbwa na mengine mengiikiwemo suala la usalama wa watoto” Amesma Issa.

Nao, baadhi ya watoto wanaoishi katika kituo wamemshukuru Nabii Suguye kwa kugushwa kwake kwa kuwapatia msaada huo, huku msimamizi wa kituo hicho akimuomba kuendele kuwa na moyo huo wa kutoa na kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu uliotupatia ni Imani yetu uzio huu utakamilika kwa akati ili nasi tuondokane na kero mbalimbali zinazotukabili,pia tukuombe uendelee na moyo huo huo wa kuwajali watu wasiojiweza” Wamesema watoto hao na msimamizi wa kituo hicho.”
Discussion
Reader comments
0 contributions