Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema katika kipindi cha mwezi Septemba 2025 hadi Septemba 2026, ofisi yake haijapokea kesi yeyote inayomhusisha mtunza kumbukumbu na nyaraka katika ofisi za umma aliyeshtakiwa kwa kukiuka maadili au kiapo chake.
Kikwete ameyasema hayo leo Septemba 23, 2026 jijini Dodoma katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA).
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa taaluma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, akieleza kuwa bila kumbukumbu sahihi na zilizohifadhiwa ipasavyo, Serikali haiwezi kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.
"Naupongeza uongozi wa TRAMPA kwa kusimamia maadili ya watendaji wenu kwa kuhakikisha wanazingatia viapo vyao katika utekelezaji wa majukumu yao,"amesema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utendaji kazi kwa watunza kumbukumbu na nyaraka nchini, huku akiwaagiza watendaji hao kutumia ipasavyo teknolojia hususani mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), katika kutunza kumbukumbu na nyaraka za Serikali ili kuzuia taarifa kutumiwa vibaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TRAMPA Taifa, Devotha Mrope ameahidi kuwa chama hicho kitaendelea kutumia weledi kuhakikisha wanachama wake wanaimarisha usiri na ulinzi wa taarifa za Serikali na watumishi wa umma.
Mrope amesema TRAMPA pia inatarajia kuona Serikali ikihimiza matumizi ya teknolojia katika utunzaji wa kumbukumbu, hususani mfumo wa ‘e-Office’, pamoja na kuanzisha vituo vya kisasa vya utunzaji wa kumbukumbu na taarifa katika maeneo mbalimbali nchini.
Discussion
Reader comments
0 contributions