Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Tabora kwa kutembelea wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua, ambako amekagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na kutoa maelekezo kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
Katika ziara hiyo, waziri Kikwete amezindua Shule ya Msingi Lolangulu Mlimani wilayani Uyui iliyojengwa kwa shilingi milioni 342.9.

Pia waziri Ridhiwani Kikwete amekagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya Kituo cha Polisi Usoke chenye thamani ya shilingi milioni 80, nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo inayogharimu shilingi milioni 280 na wodi ya watoto katika Kituo cha Afya Ulyankulu yenye thamani ya shilingi milioni 275 huku akionyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo minne yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 977.9.
Aidha amewataka wasimamizi kuhakikisha miradi ambayo haijakamilika inakamilishwa kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa, huku wananchi na viongozi wakihimizwa kuitunza na kuitumia ipasavyo miradi iliyokamilika ili iwe na tija na kutoa huduma endelevu.

Akizungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali, Waziri Kikwete amepokea hoja zilizowasilishwa na wabunge, madiwani, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi.
Hoja hizo zimehusisha uhaba wa watumishi katika sekta za afya, elimu na kilimo, changamoto za miundombinu, kuchelewa kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya maji na nishati pamoja na malalamiko kuhusu bei ya tumbaku katika masoko ya msimu huu.

Kuhusu uhaba wa watumishi, waziri Kikwete amewahakikishia kuwa Serikali imeidhinisha ajira mpya 45,000 katika kada mbalimbali, zitakazogawanywa kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika.
Aidha, ameelekeza mamlaka za utumishi, kupitia Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, kufanya msawazo wa watumishi ili kupunguza upungufu uliopo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Discussion
Reader comments
0 contributions