Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Wadau mbalimbali mkoani Shinyanga, wameunda kikosi kazi cha kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu ( ATS) na kuandaa mpango kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambao utajumuisha utoaji wa elimu kwenye jamii wakilenga kudhibiti usafirishaji huo.
Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga Issa Kisiroti ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kikosi kazi hicho amesema, mpango kazi huo umeanza rasmi Septemba 2026, ukiwa na madhumuni ya ushirikiano katika kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu , ambao ni kosa linalovuka mipaka.
"Manusura wakubwa wa usafirishaji haramu wa binadamu ni makundi ya wasichana na watoto wadogo ambao wanatumiwa kwa njia ya udanganyifu kwa lengo la wanaowatumia kujinufaisha kwa kujipatia fedha hivyo kwa kushirikiana tutaweza kutokomeza," amesema Kisiroti.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lyidia Kwesigabo (Katibu wa Kikosi Kazi) amesema, wamejengewa uwezo wa kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa lengo la kutengeneza mpango kazi .
Naye Mwajuma Ally kutoka shirika la Community of Volunteers for the World (CVM) kupitia Mradi wa emPoWeReD II wa kushirikiana na Apartnership with Africa (APA) na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Sekretarieti ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu (ATS), amesema wameamua kuunda kikosi kazi, ili kutokomeza biashara hiyo.
"Tumefanya makubaliano na kuunda kikosi kazi cha mkoa wa Shinyanga ambacho kinakwenda kutoa elimu ya uelewa maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni na kwenye jamii pia tumekuwa tukishirikiana na Chama Cha Wafanyakazi wa Hifadhi ,Hoteli,Majumbani, na Huduma za jamii na Ushauri (CHODAWU ) nakutoa elimu kwa wasichana wa kazi za nyumbani," amesema Mwajuma.
Ameongeza kuwa, kikosi kazi kitaenda kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu kwa jamii,kutambua viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu,kuzuia na kuwasaidia manusura kupata msaada stahiki .
Kikosi kazi kilichoundwa, kinajumuisha wadau mbalimbali ikiwemo Afisa Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Mwendesha Mashtaka, Hakimu Mkazi, Ustawi wa jamii, Maendeleo ya jamii, Mganga Mkuu wa Mkoa, Afisa kazi, Kiongozi wa Dini na Mwandishi wa Habari.
Discussion
Reader comments
0 contributions