Na Daniel Gahu - Katavi.
Mkoa wa Katavi umeendelea kudhihirisha nafasi yake katika kuimarisha uchumi wa kilimo baada ya kupokea ujumbe wa wataalam kutoka Mkoa wa Kigoma waliowasili kwaajili ya ziara ya mafunzo ya kujifunza namna ya uanzishaji na uendeshaji wa vituo vya kukusanyia na kuuza mazao ya mchele na muhogo.
Ujumbe huo unahusisha wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na wataalam kutoka Halmashauri ya Mji Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe.

Ujumbe huo umepokelewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Florence Chrisant, ambaye amesema kuwa ziara hiyo ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya mikoa katika kubadilishana uzoefu na kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
“Maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kupatikana kwa kufanya kazi peke yetu. Kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka maeneo yenye mafanikio ni sehemu ya safari ya kujenga uchumi imara unaotegemea kilimo chenye tija,” amesema Chrisant.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Katavi umejipanga kuhakikisha uzoefu wake katika uanzishaji wa vituo vya kukusanyia na kuuza mazao unashirikishwa kwa wadau wengine ili kuongeza thamani ya mazao na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na shughuli zao za kilimo.
Katika ziara hiyo ya mafunzo, wataalam hao watatembelea Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa lengo la kujifunza uzoefu wa uanzishaji na uendeshaji wa vituo vya kukusanyia na kuuza mazao ya mchele na muhogo.

Kwa upande wao, wataalam kutoka Mkoa wa Kigoma wameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa mapokezi mazuri na utayari wake wa kushirikiana nao katika kujenga mifumo bora ya masoko na biashara ya mazao ya kilimo.

Discussion
Reader comments
0 contributions